Serikali yaomba Wakenya kutoa msaada wa chakula kwa wathirika wa Zilizala Uturuki

"Tunaomba wenye uwezo wa kutoa msaada wa chakula, nguo, bidhaa na hata pesa kufanya hivyo," sehemu ya taarifa ilisoma.

Muhtasari

•Tetemeko la Ardhi nchini Uturuki na Syria lilijiri usiku wa Jumapili na mpaka sasa shughuli za uokoaji zinaendelea.

• Tayari watu zaidi ya elfu 7 wameripotiwa kufariki katika mkasa huo mbaya katika siku za hivi karibuni nchini Uturuki.

Majumba yakiporomoka Uturuki
Majumba yakiporomoka Uturuki
Image: BBC

Serikali ya Kenya imetoa wito kwa Wakenya wenye moyo wa kuguswa kutoa msaada wa vyakula na vitu vingine vya msaada ili kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi katika mataifa ya Uturuki na Syria.

Waziri wa masuala ya kigeni Alfred Mutua kupitia ukurasa wake wa Twitter alitoa risala zake kwa mataifa hayo huku shughuli za uokoaji zikiingia siku yake ya tatu Jumatano hii.

Vyanzo vya habari vya kimataifa vinaripoti kuwa takribani watu elfu nane wamepatikana wamefariki katika mkasa huo kwa kunaswa ndani ya vifusi vya majumba yaliyoporomoka usiku wa kuamkia Jumatatu baada ya zilizala ya kiwango cha juu kuzuka.

Mutua alionesha kuguswa kwake na kile kilichotokea huku akisema kuwa Kenya na Uturuki wanashiriki matukio sawa ambayo yametokea kipindi ambapo janga la Covid-919 limepungua.

“Tunaungana na jamii ya kimataifa kusimama na nyinyi na pia kutoa risala za rambirambi kwa familia na ndugu waliopoteza wenzao. Natoa wito kwa Wakenya wenye moyo mzuri na wenye uwezo wa kutoa msaada wa chakula, nguo, bidhaa na hata pesa kufanya hivyo ili tuwasaidie waathirika,” sehemu ya taarifa hiyo ya Mutua ilisoma.

Mutua alisema kuwa hivi karibuni watatoa taarifa Zaidi jinsi Wakenya wa kutoa msaada wataweza kufanya hivyo ili msaada huo uweze kuwafikia walioathirika na zilizala Uturuki kwa haraka.

Katika taarifa hiyo, waziri huyo alisisitiza taarifac ya katibu wa masuala ya wanaoishi nje ya nchi kwamba mpaka sasa hakuna Mkenya aliyeripotiwa kuathirika au kufariki katika mkasa huo ambao jamii ya kimataifa imejitoa kwa hali na mali kutoa msaada na kuokoa kufukua vifusi hivyo kwa haraka.