Wizara ya Afya yazindua kampeni ya chanjo ya kipindupindu kwa njia ya mdomo

Chanjo hiyo inanuia kuwalinda watu milioni 2.2 katika miji ya Nairobi, Wajir, Tana River, Garissa, na kambi za wakimbizi za Dadaab.

Muhtasari

• "Hatua hii ni sehemu kuu katika mwitikio wetu wa kina kwa mlipuko wa sasa wa kipindupindu,” - Waziri Nakhumincha.

Waziri Nakhumincha azindua chanjo ya kipindupindu
Waziri Nakhumincha azindua chanjo ya kipindupindu
Image: facebook

Wizara ya afya nchini imezindua chanjo yakujikinga dhidi ya ugonjwa wa kipindupindu, ambayo ni chanjo ya kwanza dhidi ya ugonjwa huo ambao umeripotiwa katika sehemu nyingi katika miezi ya hivi karibuni.

MoH walitangaza kwamba chanjo hiyo haitakuwa kwa njia ya sindano bali ni ya kumezwa ili kujikinga dhidi ya kipindupindu, ugonjwa ambao unaua kwa kasi chini ya saa 24 kama hautatibiwa.

Wizara ilisema kuwa chanjo hiyo itatumwa katika maeneo ya Nairobi ambako kipindupindu umeripotiwa kuwavamia watu haswa katika vitongoji duni pamoja na sehemu za Wajir, Tana River, Garissa na kwenye kambi za wakimbizi ambako maisha ni ya hali ya kuvutia kipindupindu kwa urahisi.

“Mapambano dhidi ya kipindupindu yamepata msukumo muhimu! Leo, Wizara ya Afya ilizindua kampeni ya Chanjo ya Kipindupindu kwa Njia ya Mdomo, kwa lengo la kuwalinda watu milioni 2.2 katika miji ya Nairobi, Wajir, Tana River, Garissa, na kambi za wakimbizi za Dadaab. Hatua hii ni sehemu kuu katika mwitikio wetu wa kina kwa mlipuko wa sasa wa kipindupindu,” sehemu ya ripoti hiyo ilisoma.

Shughuli ya uzinduzi wa chanjo hiyo ilifanyika katika kaunti ya Tana River na kuongozwa na waziri wa Afya, Dkt. Nakhumicha S. Wafula, ambaye alisisitiza umuhimu wa chanjo kama chombo cha kulinda watu binafsi na jamii, lakini pia alisisitiza kuwa chanjo pekee haiwezi kudhibiti ugonjwa huo.

"Ni muhimu kwamba sote tushirikiane kukuza hatua endelevu za kuzuia na kudhibiti, ikiwa ni pamoja na maji, usafi wa mazingira, na mazoea ya usafi. Chanjo itakayotumika ni salama, na ninawahimiza watu wote wanaostahiki kutumia fursa hii kulinda wao wenyewe na jamii zao" alishauri.

Wizara, kwa ushirikiano na wizara nyingine kutoka kwa kaunti zilizoathirika pamoja na wadau wa afya wamechukua hatua mbalimbali kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa juu, utoaji wa vifaa vya kipindupindu na vifaa vya Maji na Usafi wa Mazingira (WASH), na tahadhari ya dharura kwa kaunti zote.