DP Gachagua atoa wito kwa vyombo vya habari kuwa na uadililifu bila mapendeleo

Naibu Rais alidai vyombo vya habari vilieneza habari potovu wakati wa uchaguzi.

Muhtasari

•DP Rigathi  Gachagua alisema serikali ya Rais William Ruto inatambua uhuru wa vyombo vya habari.

•Alisema vyombo vya habari vikiwa na mapendeleo basi hawatakuwa na budi kukabiliana na wao kwa njia ya siasa.

Image: TWITTER// RIGATHI GACHAGUA

Naibu wa rais, Rigathi Gachagua ametoa wito kwa vyombo vya habari kudumisha uadilifu na kutekeleza majukumu yao ya kusambaza habari bila mapendeleo ya aina yoyote.

Wakati wa kikao na waandishi wa habari siku ya Jumapili, Gachagua alisema serikali ya Rais William Ruto inatambua uhuru wa vyombo vya habari na kusisitiza kuwa vyombo vya habari vina majukumu  muhimu ya kuwafahamisha na kuwafundisha Wakenya.

Naibu rais pia aliomba vyombo vya habari kuwa na uadilifu katika utendakazi wake akieleza kuwa kama walivyo na uhuru wa kuikosoa serikali, kwa upande mwingine wakubali kusifiwa wanapofanya vizuri na kukosolewa wakikosea.

"Uhuru wa vyombo vya habari lazima utumike kwa uwajibikaji. Kenya Kwanza inaheshimu vyombo vya habari ambavyo tunatazamia kukosolewa tunapokosea. Hata hivyo, vyombo vya habari pia lazima viwe tayari kukosolewa. Havipaswi kuhisi tunavishambulia." alisema Gachagua.

Kulingana na Gachagua, muungano wa Kenya Kwanza uliweza kufaulu dhidi ya vyombo vya habari msimu wa uchaguzi huku akidai kuwa viliwaunga mkono wapinzani wao katika mrengo wa Azimio- One Kenya. Gachagua alivishutumu vyombo vya habari pia kwa kuendesha kura za maoni alizodai zilikuwa za uongo wakati wa kampeni kwa kusema kuwa Raila Odinga alikuwa anaongoza.

Vile vile, naibu rais aliongeza kuwa wakati mwingine vyombo vya habari vikiwa na mapendeleo basi hawatakuwa na budi kukabiliana na wao kwa njia ya siasa  akiwahimiza wanahabari kukubali kuwa Azimio ilishindwa hivyo basi wafanye kazi yao kwa njia isiyo ya kupendelea.

Hapo awali, naibu rais na baadhi ya viongozi wa Kenya wameonekana kivikashifu vyombo vya habari. Gachagua alidai kuwa vyombo vya habari hutumiwa vibaya na "makateli' kueneza habari zinazopotosha.