Homa Bay: Mhubiri wa miaka 45 akamatwa kwa kunajisi msichana wa gredi 4

Wazazi wa mtoto huyo walimpeleka kwa kanisa la mchungaji kuombewa na kumuacha huko, muda ambao mhubiri anadaiwa kutumia fursa.

Muhtasari

• Mchungaji huyo pamoja na msichana huyo mwathiriwa ambaye alikuwa anasoma gredi 4 wote wanatoka katika kijiji kimoja.

Polisi katika kaunti ya Homa Bay wamemweka chini ya ulinzi kasisi wa kanisa moja mwenye umri wa miaka 45 kwa tuhuma za kumnajisi msichana wa miaka 16.

Inadaiwa kwamba kasisi huyo alimfanyia kitendo cha aibu msichana huyo nyumbani kwake usiku wa Jumapili wakati wa ibada ya maombi.

Mchungaji huyo pamoja na msichana huyo mwathiriwa ambaye alikuwa anasoma gredi 4 wote wanatoka katika kijiji kimoja.

Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Homa Bay Sammy Koskei katika video moja iliyopakiwa mitandaoni alidhibitisha kisa hicho na kusema kwamba uchunguzi Zaidi kubaini mazingira yaliyosababisha tukio hilo la aibu umeanzishwa.

“Tunachunguza kisa cha unajisi kilichojiri Machi 11 katika sehemu inayojulikana kama Kapita, mpaka sasa tumefanikiwa kumtia nguvuni mshukiwa, mchungaji wa kanisa liitwalo Roho, mwenye umri wa miaka 45 na alimnajisi msichana wa miaka 16 na kesi hiyo iko mahakamani,” Kamanda huyo alisema huku akitoa ushari kwa watu wa kaunti ya Homa Bay kutojihusisha katika vitendo vya mapenzi na watoto wadogo na badala yake kujihusisha kimapenzi na watu wa rika lao.

Afisa wa watoto katika kaunti ndogo ya Homa Bay Joseph Otieno alisema mama wa mwathiriwa alimwasilisha kwa maombi na kuwaacha peke yao katika hekalu hilo. Ni wakati huu ambapo mchungaji anadaiwa kumnajisi msichana huyo.