Mbunge Opiyo Wandayi atiwa mbaroni

Wandayi na Madzayo walikamatwa wakiongoza maandamano jijini Nairobi.

Muhtasari

•Wawili hao walikamatwa katika  KICC ambapo walikuwa wameungana na viongozi wengine wa mrengo wa upinzani kwa ajili ya maandamano.

amekamatwa
Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi amekamatwa
Image: JACK OWUOR

Mbunge wa eneo la Ugunja, Opiyo Wandayi na Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo wamekamatwa katikati mwa jiji la Nairobi ambako maandamano ya kupinga gharama ya juu ya maisha yanaendelea.

Wawili hao walikamatwa katika  KICC ambapo walikuwa wameungana na viongozi kadhaa wa mrengo wa upinzani kwa ajili ya maandamano.

Waandamanaji kadhaa pia walikamatwa kutoka pembe tofauti za mji mkuu katika juhudi za kuzuia machafuko. Maafisa wa polisi walilazimika kuwarushia vitoa machozi waandamanaji kwa nia ya kuwatawanya.

Machafuko makubwa yalishuhudiwa katika baadhi ya maeneo ya Kibera huku baadhi ya waandamanaji wakionekana wakikabiliana na maafisa wa GSU ambao walikuwa wakiwarushia vitoa machozi. Barabara zote zinazoelekea Ikulu zimekuwa chini  ya ulinzi mkali kuanzia mapema Jumatatu asubuhi.

Maandamano yanaendelea jijini Nairobi huku waandamanaji wakisubiri kuwasili kwa Raila Odinga ambaye katika chapisho la facebook alisema kuwa ameona kazi imeanza na yu njiani akielekea kule.