Polisi waimarisha ulinzi ili kukabiliana na waandamanaji wanaozua ghasia

Polisi wameweka ulinzi katika sehemu tofauti za nchi kufuatia maandamano yaliyotangazwa na Raila.

Muhtasari

•Jumatatu asubuhi , kulishuhudiwa makundi ya polisi wakiwa wamejihami ili kudhibiti rabsha yoyote ambayo ingeweza kuzuka. 

•Barabara inayoelekea ikulu imewekewa ulinzi ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atafika katika makao ya rais kwa njia ya vurugu.

wameimarisha ulinzi jijini Nairobi mnamo Machi 20, 2023.
Polisi wameimarisha ulinzi jijini Nairobi mnamo Machi 20, 2023.
Image: EZEKIEL AMINGA

Polisi wameweka ulinzi mkali katika sehemu tofauti za nchi kufuatia maandamano yaliyotangazwa na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga .

Jumatatu asubuhi , kulishuhudiwa makundi ya polisi wakiwa wamejihami ili kudhibiti rabsha yoyote ambayo ingeweza kuzuka. 

Bw Odinga alitangaza maandamano ya umma nchini kote kumpinga rais William Ruto.

Akizungumza jijini Nairobi siku ya Jumapili, Odinga aliwaambia wafuasi wake wakutane katikati mwa jiji la Nairobi wakianza na KICC.

Alisema kuwa baadaye wataenda hadi kwenye ikulu ya rais ya Nairobi.

Jambo hili halikuchukuliwa kwa wepesi na polisi ambao wamehakikisha wameimarisha usalama katika sehemu nyingi za nchi.

Katika jiji la Kisumu, Polisi wameweka ulinzi dhabiti kwa barabara inayoelekea ikulu ya Kisumu huku baadhi ya wanabiashara wakiogopa kufungua biashara zao kwa hofu ya vurugu wakati wa maandamano hayo.

Jijini Nairobi,usalama umewekwa katika ofisi za kiserikali kama vile KICC na mahakama ya juu ili kuzuia mtu yeyote kufikia mazingira hayo ikifuatia tangazo la Odinga kuwa wataanza kwa kukutana KICC.

Barabara inayoelekea ikulu ya Nairobi pia imewekewa ulinzi ili kuhakikisha kuwa hakuna mtu yeyote atafika katika makao ya rais kwa njia ya vurugu.

Waziri wa usalama na maswala ya ndani, Kithure Kindiki alitangaza kuwa Ikulu ni sehemu inayolindwa hivyo hakuna anayeruhusiwa kuleta vurugu karibu na eneo hilo

Bustani la Jevanjee imedhibitiwa na polisi na hakuna anayeruhusiwa kuingia humo ndani. Katika eneo la Kibra ,tayari polisi walianza kukabiliana na waandamanaji waliojaribu kuzua rabsha na kuwakamata baadhi yao.

Huku haya yakiendelea,sehemu zingine nchini kama Mombasa zimeshuhudia utulivu na biashara kama kawaida.

Raila Odinga anatarajiwa kutoa mwelekeo wa  shughuli ya siku ya Jumatatu.