AU yataka Ruto Raila kufanya mazungumzo

AU ilisema itaunga mkono serikali katika kuendeleza umoja

Muhtasari

• Maandamano yalizua ghasia ikiwemo kuuawa kwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno.

Muungano wa Afrika (AU) umetoa wito wa kufanyika mazungumzo kati ya viongozi nchini Kenya ili kukuza umoja na maridhiano ya kitaifa.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne, mwenyekiti wa AU Moussa Faki aliahidi kuunga mkono serikali katika juhudi zake za kuendeleza umoja wa kitaifa, amani na utulivu.

"AU inaelezea wasiwasi wake mkubwa kutokana na ghasia kufuatia maandamano ya umma nchini Kenya tangu Machi 21, 2023, ambayo yalisababisha watu kupoteza maisha, uharibifu wa mali na kukatizwa kwa shughuli  za kiuchumi huko Nairobi," alisema. 

"Ninawaomba wahusika wote kuwa watulivu na kushiriki katika mazungumzo ili kutatua tofauti zozote zinazoweza kuwepo kwa maslahi ya umoja na maridhiano ya kitaifa,"Faki alisema.

Hii ni baada ya Azimio kuitisha maandamano kote nchini kupinga kupanda kwa gharama ya maisha miongoni mwa masuala mengine. Waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano kufuatia mwito wa kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

Viongozi wa makanisa pia wameutaka upinzani kusitisha maandamano hayo, na kuwataka viongozi kushiriki katika mazungumzo. Hata hivyo, Raila ameshikilia kuwa maandamano hayo yataendelea hadi Rais William Ruto atakaposhughulikia matakwa yao.

Kufuatia maandamano ya kwanza ya Azimio mnamo Machi 20, Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja alisema kaunti hiyo ilipoteza takriban Shilingi milioni 40.

Baada ya maandamano hayo ya Jumatatu, maafisa wa polisi wasiopungua 20 walijeruhiwa katika makabiliano na waandamanaji katika baadhi ya maeneo ya Nairobi.

Polisi walisema gari lao moja liliteketezwa na mengine mawili kuharibiwa katika machafuko yaliyoshuhudiwa katika maeneo ya Kawangware, Huruma, Makongeni na Dandora. Pia, msikiti na kanisa moja viliteketezwa katika mtaa wa Kibera huku takriban watu watatu wakiripotiwa kupigwa risasi mjini Kisumu.