Seneta Boni Khalwale atofautiana na rais Ruto kuhusu kubinafsishwa kwa makampuni

Seneta huyo wa UDA ndiye kiongozi wa hivi punde zaidi kupinga mipango ya kubinafsisha mashirika ya umma.

Muhtasari

• Alizungumza Jumamosi katika eneo bunge la Malava ambapo makanisa yaliandaa ibada ya shukrani.

• Naibu Rais Rigathi Gachagua ni miongoni mwa viongozi wakuu waliohudhuria hafla hiyo.

Seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale
Seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale
Image: MAKTABA

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amepinga mipango ya kubinafsisha kampuni za sukari za Mumias na Nzoia.

Khalwale alisema serikali haifai kuachia viwanda vya sukari akisema viwili hivyo ni kiini cha jamii ya Waluhya.

Alisema jamii ya Waluhya inajivunia mashamba hayo na kwamba walitoa ardhi ya mababu zao ili kuwa na sukari ya Mumias na Nzoia Magharibi mwa Kenya.

“Mimi kama Kiongozi wa jamii ya waluhya, Babu zetu walipeana hekta 12,500 za kampuni ya Mumias Sugar na wakapeana hekta 24,500 za kampuni ya sukari ya Nzoia. Ukibinafsisha mtu ataondoka na ardhi ya mababu zetu. Sisi hatuezi unga mkono. Hatuwezi,"  alisema.

Alizungumza Jumamosi katika eneo bunge la Malava ambapo makanisa yaliandaa ibada ya shukrani.

Naibu Rais Rigathi Gachagua ni miongoni mwa viongozi wakuu waliohudhuria hafla hiyo.

Khalwale aliendelea kuitaka serikali kufanyia kazi changamoto zinazovikabili viwanda vya sukari badala ya kuvibinafsisha.

"Hii si kwa sababu ya kutomheshimu rais na serikali. Hicho ndicho kidogo tulichonacho katika uchumi wa sekta ya sukari," alisema.

Alisema changamoto halisi ni uagizaji wa Sukari kutoka nje ambayo inaweza kutatuliwa kwa urahisi.

Seneta ndiye kiongozi wa hivi punde zaidi kupinga mipango ya kubinafsisha mashirika ya umma.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga pia alikashifu hatua ya Baraza la Mawaziri kumpa Waziri wa Hazina Njuguna Ndung'u mamlaka ya kubinafsisha mashirika ya serikali.

Baraza la Mawaziri liliidhinisha Mswada wa Ubinafsishaji, 2023 ambao utabatilisha Sheria ya Ubinafsishaji ya 2005.

Raila alisema mchakato wa ubinafsishaji haukufuata uangalizi kwa vile haukupitia Bunge.

"Kwa upande mwingine, wanataka kuuza biashara za serikali bila kupita Bungeni. Serikali inataka kuuza kampuni za umma kwa watu wao. Tunasema hapana," Raila alisema.

Raila alisema kuwa serikali haiwezi kuuza mali ya umma bila idhini ya Bunge.