DCI yaomba umma kutoa taarifa za majambazi waliovamia studio za redio Nakuru

Genge hilo la watu wanne wafisadi lilichukua simu 8, pesa taslimu zaidi ya Sh35,000 na jozi nane za viatu.

Muhtasari

• Kamera tano pia ziliharibiwa na majambazi hao kabla ya kutoroka kwa kuruka eneo la jengo hilo.

DCI yatoa wito kwa umma kutambua majambazi waliovamia redio huko Nakuru.
DCI yatoa wito kwa umma kutambua majambazi waliovamia redio huko Nakuru.
Image: DCI//FACEBOOK

Maafisa wa upelelezi wa jinai DCI kaunti ya Nakuru wametoa ombi kwa umma kutoa taarifa zozote zitakazopelekea kukamatwa kwa majambazi watatu waliovamia kituo cha redio jijini humo na kufanya wizi wa bidhaa.

Kupitia taarifa ya hivi punde, DCI waliomba umma kutoa taarifa kuhusu watu hao ambao walionekana kwenye video iliyonaswa na CCTV lakini pia na Facebook ambapo kipindi cha redio kilikuwa kinapeperushwa moja kwa moja.

Katika tukio hilo la kusikitisha lililorekodiwa moja kwa moja na kamera, majambazi hao waliokuwa na silaha za moto na mapanga walinaswa walipokuwa wakiingia kwenye studio ya Mwinjoyo FM, ambapo waliwaamuru watangazaji walale chini kabla ya kupora mifuko yao kwa ajili ya kutafuta fedha na vitu vinginne vya thamani.

“Zima kitu hicho! Lala chini,” mmoja wao aliamuru huku watangazaji wawili walioshtuka mwanamume na mwanamke wakiruka chini.

Majambazi hao ambao walikuwa wameficha nyuso zao kwa kutumia hancifu walikatiza utangazaji wa moja kwa moja wa Kigocho, uliomshirikisha mwanamuziki wa injili Robert Kiarie.

Genge hilo la watu wanne wafisadi lilichukua simu 8, pesa taslimu zaidi ya Sh35,000 na jozi nane za viatu. Kamera tano pia ziliharibiwa na majambazi hao kabla ya kutoroka kwa kuruka eneo la jengo hilo, lililo katika vitongoji vya kifahari vya Nakuru Milimani.

Msako wa kuwasaka majambazi umeanzishwa na tunaomba taarifa kutoka kwa yeyote anayeweza kuwatambua majambazi waliovalia nguo nyeusi ajitolee kwetu bila kujulikana kupitia kwa namba zetu, DCI iliomba.