Waziri wa Afya awaagiza wafanyikazi wote wa KEMSA kurejea kazini

Takriban wafanyikazi 200 wamekuwa wakifanya kazi kutoka nyumbani kwa zaidi ya miaka miwili.

Muhtasari

• Wale waliofanya kazi nyumbani kwa miezi 19 walilipwa milioni 45 kila mwezi na kufikia jumla ya  milioni 855.

 

Waziri wa Afya Susan Wafula akiwasalimia maafisa wizara ya afya wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Kemsa katika bohari ya Embakasi Mei 18,2023.
Waziri wa Afya Susan Wafula akiwasalimia maafisa wizara ya afya wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Kemsa katika bohari ya Embakasi Mei 18,2023.
Image: MAGDALENE SAYA

Waziri wa Afya Susan Nahumicha amemuagiza afisa mkuu mtendaji wa Kemsa Andrew Mulwa kuhakikisha wafanyikazi wote wameripoti kazini Ijumaa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bodi mpya ya Kemsa siku ya Alhamisi, Nahumicha alisema ni ishara ya kutoajibika ikiwa zaidi ya wafanyikazi 200 wamekuwa wakifanyia kazi nyumbani kwa zaidi ya miaka miwili ilhali wanaendelea kulipwa mishahara.

Haya yanajiri baada ya taarifa kuwa kampuni ya KEMSA kufikia sasa imelipa mamilioni ya pesa kwa zaidi ya wafanyikazi 300 ambao walikuwa wameamrishwa kufanyia kazi nyumbani baada ya sakata ya Covid-19.

Radio Jambo imeona nyaraka zinazoonyesha kuwa kundi la wafanyakazi 350 wa Kemsa walioagizwa kufanya kazi wakiwa nyumbani waliendelea kupokea mishahara yao.

Nyaraka hizo zilifichua kwamba waliochukua nafasi za waliokuwa wakifanya kazi nyumbani walipata mishahara na marupurupu makubwa hata baada ya mikataba yao kukamilika.

Wale waliofanya kazi nyumbani kwa miezi 19 walilipwa milioni 45 kila mwezi na kufikia jumla ya  milioni 855.

Hata hivyo, Waziri katika mahojiano na runinga moja hapa nchini alifafanua kwamba wafanyikazi waliokuwa wakifanya kazi kutoka nyumbani walilipwa nusu ya mishahara yao inavyotakikana kwa mujibu wa sheria za kazi.

Hakuna uharamu wafanyikazi waliosimamishwa kupokea nusu ya mishahara yao.