Tunataka BBI iendelee-Uhuru Kenyatta

Alisema ripoti kwamba BBI ilikusudiwa kuongeza muda wake ni za uongo.

Muhtasari
  • Uhuru aliitetea BBI hadharani akibainisha kuwa mpango huo ulikusudiwa kuweka pesa nyingi zaidi mifukoni mwa wananchi wa kawaida.
RAIS MSTAAFU UHURU KENYATTA WAKATI WA KONGAMANO LA KITAIFA LA JUBILEE 22/05/2023
Image: EZEKIEL AMING'A

Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta amesema Chama cha Jubilee bado kinaendelea na mpango wa BBI.

Akizungumza wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe lililofanyika katika uwanja wa Ngong Racecourse, Uhuru alisema kuwa suala la BBI ni kwa ajili ya maslahi ya Wakenya pekee, na wala si kwa ajili ya kujinufaisha binafsi.

“Tulikua tunataka mambo ya BBI yatendeke na bado tunataka yatendeke, tulikua tunatetea mambo ya Kenya,” alisema.

Pia alisema ishara ya Chama cha Jubilee ni njiwa inayoashiria amani na inafaa kusalia hivyo.

“Sisi tunataka mambo ya wakenya, hatutaki jamii kupigana,” aliongeza.

Mnamo Agosti 2022, miezi kadhaa baada ya Mswada wa Marekebisho ya Katiba 2022 kutangazwa kuwa kinyume cha katiba, Uhuru alisema BBI ilikusudiwa kuleta mabadiliko na sio kuongeza muda wake wa kukaa ofisini kama inavyodaiwa na wapinzani wake.

Alisema ripoti kwamba BBI ilikusudiwa kuongeza muda wake ni za uongo.

"Lengo langu halikuwa kuendelea kuwa madarakani, nilitaka mabadiliko ya watu tu lakini propaganda zikaenezwa kuwa nataka kuendelea kuwa madarakani na watu wengi waliamini nadharia hiyo," alisema.

Uhuru aliitetea BBI hadharani akibainisha kuwa mpango huo ulikusudiwa kuweka pesa nyingi zaidi mifukoni mwa wananchi wa kawaida.

"Tulikosea wapi mimi na Raila tulipokuja na BBI? Kama tulivyosema awali, tunataka pesa za serikali ziingie mifukoni mwa mwananchi na zisigawiwe ng'ombe, mbuzi na mchanga," alisema.

Rais alisema baadhi ya waliopinga waraka huo akiwemo Rais William Ruto walihusika kuitayarisha.