Ruto na Raila wakikutana ana kwa ana watapata suluhu-Atwoli

Atwoli hata hivyo ametetea pendekezo la Hazina ya Makazi inayopendekezwa, akisema kuwa itaondoa makazi duni

Muhtasari
  • Atwoli badala yake anawataka viongozi hao wawili kuondoa tofauti zao kibinafsi na kuiongoza nchi kuelekea kuimarika kwa uchumi.
Bosi wa COTU Francis Atwoli
Bosi wa COTU Francis Atwoli
Image: MAKTABA

Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli sasa anamtaka Rais William Ruto na kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga kuachana na mchakato wa mazungumzo ya pande mbili unaonuiwa kutatua tofauti kati ya upinzani na serikali.

Atwoli badala yake anawataka viongozi hao wawili kuondoa tofauti zao kibinafsi na kuiongoza nchi kuelekea kuimarika kwa uchumi.

Akizungumza wakati wa hotuba kwa wanahabari siku ya Alhamisi, bosi huyo wa COTU alimwaga maji baridi kwenye mazungumzo yanayoendelea akisisitiza kwamba hayana umuhimu wa kuunganisha nchi.

"Ile jopo halina maana yoyote, ni juu ya mheshimiwa Raila Amolo Odinga, William Samoei Ruto kukutana na watu wawili waangalie ni njia gani kwa sababu ni wadau katika nchi hii, ni vingozi kivyao," Atwoli alisema.

“Wale watu katika kazi na watu wa chini sana. Hawafai wakutane wawaambie hii njia ndio mwafaka. Wawili hao wanapokutana, wanaweza kupata suluhu watakapokutana."

Alisema wafanyikazi wa Kenya wameathiriwa zaidi na nyakati za kiuchumi zilizopo na wanakabiliwa na hatari kubwa kama vile kupunguzwa kazi, akiongeza kuwa ni viongozi wawili pekee wanaoshikilia suluhu la kukomesha hili kutokea.

"Si lazima kuwe na handshake, lakini kwa manufaa ya wote wa nchi hii, ni lazima waje pamoja na kuwaambia watu hapa ndipo tuko, tunawezaje kuokoa nchi hii?" Aliongeza.

"Hakuna njia ya kutoroka kwa viongozi wa upinzani au walio serikalini au wafanyikazi...hakuna njia tutapona bila kuja pamoja."

Matamshi hayo yalijiri baada ya Muungano wa Wazalishaji wa Kenya kutoa wito kwa Bunge kughairi Mswada wa Fedha wa 2023, kikisema kuwa nchi inaweza kupoteza Ksh.135 bilioni na kuteseka zaidi ya watu 100,000 walioachishwa kazi.

Atwoli hata hivyo ametetea pendekezo la Hazina ya Makazi inayopendekezwa, akisema kuwa itaondoa makazi duni na pia kuhakikisha hali bora ya maisha kwa Wakenya.