Siaya: Mwili wa mtoto wa Grade 2 wapatikana ukining'inia kwenye paa la nyumba yao

Mamake alisema aliondoka kwenda sokoni na kumuacha mwanawe akicheza na dadake mdogo kabla ya kupigiwa simu kuwa amepatikana ananing'inia kwenye paa.

Muhtasari

• Mama alikataa kuamini kwamba kwamba huenda mwanawe alijitia kitanzi na kudai kwamba huenda kuna mtu alimnyonga na kuifanya iwe kama alijinyonga.

Kitanzi
Kitanzi
Image: HISANI

Mwili wa mtoto wa Grade 2 katika kaunti ya Siaya umepatikana ukiwa unaning’inia kutoka kwenye paa la nyumba yao.

Kulingana na taarifa za Citizen, familia hiyo katika kijiji cha Alego Usonga wanaendelea kuomboleza kwa kutoamini baada ya mwana wao kupatikana amening’inia kwenye paa katika chumba kimoja katika kile ambacho kinakisiwa kuwa ni kujitia kitanzi.

Kulingana na Chifu wa lokesheni ndogo ya Karapul, Dorcas Olombo, wazazi wa mvulana huyo walikuwa mbali na walishtuka walipoitwa na majirani ambao waliwafahamisha kwamba mwili wake ulikuwa ukining’inia kwenye paa, Citizen wanaripoti.

Bi Olombo aliambia Citizen kwamba mamake mtoto huyo alisimulia kwamba alikuwa ameenda sokoni na kumwacha pamoja na dadake mdogo wakicheza, ndipo aliporudi kuona maiti yake ikiwa imening'inia kwenye paa la nyumba.

Msimamizi huyo alisema kuwa mama wa marehemu alipuuzilia mbali uwezekano kwamba angeweza kujiua, kwa madai kwamba mwanawe angeweza kuuawa na mtu asiyejulikana kisha akaifanya ionekane kama kujiua.

 

Msimamizi huyo alieleza kuwa polisi walitembelea eneo la tukio na kuuchukua mwili huo hadi katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Siaya ili kusubiri uchunguzi wa maiti hiyo huku uchunguzi ukianza kuhusu kisa hicho.