Mahakama yatupilia mbali amri ya kufungwa kwa akaunti za benki za msajili mkuu wa mahakama Ann Amadi

Jaji Alfred Mabeya ameamua kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha Amadi ilinufaika na milioni 100 zinazodaiwa kulipwa na kampuni moja ya Dubai kwa ununuzi wa dhahabu.

Muhtasari

• Hata hivyo, hakimu alitupilia mbali maombi ya Amadi ya kufuta mbali kesi dhidi yake na wengine wawili - Brian Ochieng na wakili mwingine.

Msajili Mkuu wa Mahakama Ann Amadi
Image: DOUGLAS OKIDDY

Msajili Mkuu wa mahakama Ann Amadi amepata afueni baada ya mahakama kuu kutupilia mbali amri ya kufungwa kwa akaunti zake za benki.

Jaji Alfred Mabeya ameamua kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Amadi ilinufaika na dola milioni 100 zinazodaiwa kulipwa na kampuni moja ya Dubai kwa ununuzi wa dhahabu.

"Hakuna chochote kinachoonyesha kuwa mshtakiwa wa kwanza (Amadi) alihusika katika shughuli za kila siku za kampuni ya mawakili au ushahidi wa kuonyesha kwamba alinufaika na fedha hizo," mahakama ilisema.

Jaji Mabeya alisema mwanawe Brian Ochieng anafaa kubeba msalaba wake mwenyewe kwa sababu yeye ni mtu mzima na Amadi kuwa mamake haimaanishi kwamba analazimika kubeba mzigo huo kwa niaba yake.

Hata hivyo, hakimu alitupilia mbali maombi ya Amadi ya kusitisha kesi dhidi yake na wengine wawili - Brian Ochieng na wakili mwingine.

Hakimu alisema Amadi atasalia kuwa mshtakiwa katika kesi hiyo kwani Demetrios Bradshaw alikuwa sawa kisheria kumshtaki ili kuonyesha kwamba kampuni ya mawakili imesajiliwa kwa jina lake.

Katika kesi hiyo, Amadi, mwanawe Ochieng, rais wengine wawili wa Kenya na mmoja wa  Liberia wameshtakiwa na Bruton Gold Trading LLC, kwa madai kwamba kampuni hiyo ilipoteza dola 742,206.

Kampuni hiyo inadai kuwa pesa hizo zilikusudiwa kununulia dhahabu ambazo hazikufikishwa kwao Dubai.