• Kufikia sasa polisi wamewakamata washukiwa wawili ambao wanadaiwa kuhusika na kutoweka kwa Jane Mwende.
•Washukiwa hao walikamatwa Jumamosi jioni baada ya polisi kupata taarifa kuwa, Mwende angetoweka kwa sababu ya penzi.
Kisa cha kutoweka kwa Jane Mwende, ambaye ni msusi katika eneo la Mlolongo sasa kimeibua maswali chungu nzima.
Maafisa wa polisi katika eneo la Mlolongo, wameanzisha uchunguzi ili kubaini kiini cha kutoweka kwa Jane, mwanamke mwenye umri wa miaka 28 ambaye hajaonekana tangu mnamo Agosti 25 baada ya kupigiwa simu.
Kufuatia uchunguzi , polisi wamewakamata washukiwa wawili ambao wanadaiwa kuhusika na kutoweka kwa mwanadada huyo.
Washukiwa hao walikamatwa Jumamosi jioni baada ya polisi kupata taarifa kuwa, mwende huenda alitoweka kwa sababu ya penzi la mtu mmoja anayefahamika kama Januaris Musau almaarufu Shady. Mwanamke mwingine katika eneo hilo anayetambulika kama Phylis Mbithi anafuatiliwa na polisi.
Kufikia sasa polisi wanawasaka washukiwa wengine wawili, ambao wanashukiwa kuhusika na kutoweka kwa Jane Mwende.
Mnamo Agosti 25, Mwende alikua na shughuli nyingi za kutoa huduma katika saluni ya urembo na vipodozi ambapo alipokea simu.
Wenzake katika saluni hiyo wanasema alipokea simu kutoka kwa nambari isiyojulikana, na alipotoka nje kuijibu hakurudi tena.
Winnie Munyau,mmoja wa wafanya kazi katika saluni hiyo, alisema hawajawai kumuona tangu alipotoka kujibu simu walioichukulia kuwa ya mteja.
"Alipokea simu ikionekana kutoka kwa mteja na akatoka nje.Hatujawahi kumuona tangu wakati huo, na wala hakuja kazini siku iliyofuata,"
Familia na marafiki wamesema wameingia katika vituo vingi vya polisi, hospitali na vyumba vya kuhifadhia maiti wakimtafuta bila kufanikiwa.
Jennifer Mwende, Mfanyakazi mwenza aliongeza kusema;
"Hakutuambiwa chochote, alitoka akizungumza na simu, na hiyo siku kulikuwa na hitilafu ya umeme hivyo tukadhani simu yake ilikua imezima tukaamua kumsubiri ila hakurudi,"
Hali ya shaka ilitanda wakati ambapo Mwende hakurejea kazini asubuhi iliyofuata, aidha maji yalizidi unga wakati ambapo hakuenda kumchukua mwanawe kutoka shuleni.
Kufikia sasa Mwende, hajulikani aliko, polisi wakiahidi uchunguzi wa kina kubaini aliko.