Gari imetosha!Raila asema huku akifichua sahihi milioni 10 zimekusanywa

Mnamo Julai 11, Odinga alizindua tovuti ya umma kwa ajili ya kukusanya sahihi milioni 10.

Muhtasari
  • Raila ambaye alitaja uongozi wa Kenya Kwanza katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kuwa mbaya kwa nchi, alishutumu serikali kwa matumizi yasiyodhibitiwa na kukopa.
  • Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa Rais Ruto anafanya kinyume kabisa na ahadi alizotoa kwa nchi wakati wa kampeni

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga Jumamosi alifichua kuwa zaidi ya sahihi milioni 10 zimekusanywa tangu zoezi hilo kutekelezwa Julai 11.

Odinga alisema sahihi zilizokusanywa zinatosha.

"Vile mnavojuwa tumekuwa tukisanya sahihi kutoka kwa wananchi. Saa hii tumeshafika milioni kumi na zaidi sasa imetosha gari na jua yale tutafanay na hizo sahihi," Odinga alisema.

Aliongeza: “Safari hii hatutawaambia Wakenya warudi mitaani. Hapana. Watakaporudi watafanya hivyo kwa misingi mingine ambayo sitaki kufichua kwa sasa.”

Mnamo Julai 11, Odinga alizindua tovuti ya umma kwa ajili ya kukusanya sahihi milioni 10.

Hatua hiyo ni katika jitihada za kupata uungwaji mkono wa umma kwa kampeni yao kali dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.

Akihutubia wanahabari Ijumaa, Odinga alidai kuwa Rais William Ruto ameongeza matumizi ya serikali kwa Sh400 bilioni katika mwaka uliopita.

Raila ambaye alitaja uongozi wa Kenya Kwanza katika kipindi cha miezi 12 iliyopita kuwa mbaya kwa nchi, alishutumu serikali kwa matumizi yasiyodhibitiwa na kukopa.

Kiongozi huyo wa upinzani alisema kuwa Rais Ruto anafanya kinyume kabisa na ahadi alizotoa kwa nchi wakati wa kampeni