- Akizungumza na vyombo vya habari, Muheria alisema kuwa Wakenya maskini wanaendelea kubanwa kwa sababu wamebanwa kila mahali.
Askofu Mkuu wa Nyeri Anthony Muheria ameitaka Serikali kutafuta suluhu kupitia majadiliano kuhusiana na gharama ya juu ya maisha na ongezeko la gharama ya mafuta.
Akizungumza na vyombo vya habari, Muheria alisema kuwa Wakenya maskini wanaendelea kubanwa kwa sababu wamebanwa kila mahali.
“Tunatakiwa kushughulikia suala zima la nishati, mafuta na umeme, inasikitisha tumeshuhudia ongezeko la bei ya mafuta, jambo hili litaathiri mwanainchi wa kawaida katika suala la bei ya nauli,” alisema.
"Itakuwa na athari mbaya sana. Bei zote za bidhaa zitaathirika."
Aliongeza kuwa bei ya mafuta taa iliyoongezwa kwa Sh33 imeathiri maskini pekee kwani matajiri hawatumii mafuta taa kamwe.
"Lazima kuwe na masuluhisho mengine zaidi ya kusukuma na kudai nyongeza kutoka kwa yale ambayo hayapo miongoni mwa maskini. Shida za maskini zisiwe za maneno tu, lazima tuhakikishe hawakosi chakula mezani," alisema.
"Lazima tufanye majadiliano na tupate masuluhisho."
Siku ya Alhamisi, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli ilitangaza bei mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa, ikisema sasa zitauzwa kwa zaidi ya Sh200.