Mama ya mshukiwa wa mauaji ya Eric Maigo hatimaye amwaya mtama

Mtoto huyo ambaye alikamatwa Jumanne usiku amezuiliwa kwa siku 21 akisubiri uchunguzi.

Muhtasari
  • Kisha akarudi nyumbani, akafunga mlango na kuchukua godoro lake katika ishara wazi kwamba alikuwa tayari kulala.
  • Hata hivyo, inashukiwa kwamba alitoka nje ya nyumba kwa siri karibu usiku wa manane wakati kila mtu alikuwa amelala.
Mwanamke asakwa na DCI kuhusiana na mauaji ya mkurugenzi wa  fedha wa Nairobi hospital
Image: DCI/X

Familia ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya kaimu Mkurugenzi wa Fedha wa Hospitali ya Nairobi hospital Eric Maigo imevunja ukimya wake kuhusu suala hilo.

Akizungumza na NTV, mama huyo alisema kuwa siku hiyo ya maafa, bintiye alikuwa amekaa nyumbani kwao ambapo waligombana kwa ajili ya chakula majira ya saa 10 jioni.

Ili kuepusha ugomvi na mabishano zaidi kati yao, aliamuru mtoto huyo angoje na kumruhusu aendelee na kazi za nyumbani.

“Nikamwambia kama ungekuwa mtu wa kupigwa ningekupiga nikikuuliza kitu na husemi na wewe ndie ulishinda kwa nyumba. Kidogo akaanza kuongea ndio nikamwambia usifanye nikuwe na hasira na kisirani zenye zangu na wewe kaa tu huko nje nimalizane ndio urudi,” mamake aliambia NTV.

Mtoto huyo alitii maagizo ya mama yake hadi pale alipomaliza kupika.

Kisha akarudi nyumbani, akafunga mlango na kuchukua godoro lake katika ishara wazi kwamba alikuwa tayari kulala.

Hata hivyo, inashukiwa kwamba alitoka nje ya nyumba kwa siri karibu usiku wa manane wakati kila mtu alikuwa amelala.

“Sasa mimi nikapika ikaiva ako tu huko nje, kumaliza chakula akakuja akapata tushamaliza kukua mimi nikaamka nikaenda kwa chumba cha kulala. Nikaona ameingia kama anafunga mlango akatoa godoro, mimi nikaacha kama nimejua mtu anataka kulala sasa pia mimi nikalala tu nikawachana na yeye,” alisema mama.

Aliongeza: “Mimi nilijua mtu amelala kwa nyumba. Asubuhi ndio wanaamka saa kumi na mbili watoto wananiambia hayuko, nikasema asubuhu ameamka ameenda wapi.”

Mtoto huyo ambaye alikamatwa Jumanne usiku amezuiliwa kwa siku 21 akisubiri uchunguzi.

Polisi walisema mshukiwa huyo, ambaye ni mtoto mdogo anayeaminika kuwa na umri wa kati ya miaka 15 hadi 17, amekuwa akitoroka tangu wiki iliyopita Alhamisi.

Alikamatwa katika vitongoji duni vya Kibera, Nairobi katika operesheni iliyoongozwa na idara ya upelelezi ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI).

Maigo alipatikana akiwa na majeraha 25 ya kuchomwa visu katika makazi yake ya Woodley Estate wiki jana.