Babu Owino asimulia safari ya ukombozi baada ya kutumia mihadarati

Mbunge huyo alisema aliachana na dawa za kulevya Januari 2020 na amekuwa na akili timamu tangu wakati huo.

Muhtasari

• Katika mahojiano na Wakenya, alisema kuwa hakujutia mtindo wake wa maisha wa zamani kwani alikuwa bado mchanga na alitaka kuchunguza na kujionea matukio ya maisha.

 

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, amefichua kwamba alikuwa akipambana na uraibu wa dawa za kulevya wakati wa safari yake ya kuwa mbunge.

Katika mahojiano na Wakenya, alisema kuwa hakujutia mtindo wake wa maisha wa zamani kwani alikuwa bado mchanga na alitaka kuchunguza na kujionea matukio ya maisha.

“Sijutii kuwa katika maisha hayo kwa sababu sasa yamenifanya nione si vizuri kujihusisha na maisha ya aina hiyo,” alisema.

Alifunguka kwa kutumia pombe, kutafuna miraa, kutumia kokeni, kuvuta bangi, kunywa chang’aa, busaa na muratina – kwa ufupi kutumia kila aina ya dawa za kulevya.

"Baada ya kufanya haya yote, nilifanya uamuzi na kusema kwamba inatosha, na nilihitaji kusonga mbele, nilifanya uamuzi wa kuwacha kutumia pombe na dawa za kulevya. ”

Mbunge huyo alisema aliachana na dawa za kulevya Januari 2020 na amekuwa na akili timamu tangu wakati huo.

Utumizi mbaya wa dawa za kulevya na ulevi ni shida ya maisha ya vijana wengi, licha ya juhudi za kuzuia uraibu huo.

Baadhi ya waraibu hulewa sana na pombe na dawa za kulevya hivi kwamba mara nyingi hupoteza kazi au kuacha shule, hasa katika vyuo  vikuu.

Vijana ambao wamefanikiwa kujinasua kutoka kwa uraibu wametoa wito kwa wengine kujiepusha na dawa za kulevya, huku juhudi kubwa zikiwekwa ili kupambana na utumiaji.

Vijana waliorekebishwa kwa mafanikio wametoa  ushuhuda wao wa kuhuzunisha za uraibu na jinsi maisha yao yamebadilika.

Serikali, ikishirikiana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Pombe na dawa za Kulevya (NACADA), imechukuwa mtazamo tofauti wa kampeni dhidi ya unywaji pombe na dawa za kulevya, kutokana na nia njema ya viongozi.