Jalang'o atoa taarifa kuhusu afya yake wiki 6 baada ya kufanyiwa upasuaji

Jalang'o alionekana kuweza kusogeza miguu yake vizuri, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo hangeweza.

Muhtasari

•Mbunge huyo wa Lang'ata alichapisha video yake akifanya mazoezi na kunyoosha miguu yake huku akisaidiwa na mikongojo.

•Mguu wake wa kushoto bado ulikuwa umefungwa kwa plasta na alikuwa na mikongojo ya kumsaidia kusimama na kutembea.

Image: INSTAGRAM// JALANG'O

Mbunge wa Lang’ata, Phelix Odiwour almaarufu Jalang’o ametoa taarifa nyingine kuhusu maendeleo yake ya kiafya wiki kadhaa baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu.

Jalang’o alifanyiwa upasuaji mwishoni mwa mwezi Septemba baada ya kupata jeraha kwenye mguu wake wa kushoto alipokuwa akifanya mazoezi ya mpira wa vikapu.

Siku ya Jumanne, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alichapisha video yake akifanya mazoezi na kunyoosha miguu yake huku akisaidiwa na mikongojo.

"Napata nafuu.. Kweli nimepona, nasubiri tu ripoti ya madaktari," Jalang'o aliandika kwenye video hiyo.

Katika video hiyo, mbunge huyo wa muhula wa kwanza alionekana kuweza kusogeza miguu yake kwa urahisi, tofauti na ilivyokuwa wiki kadhaa zilizopita ambapo hangeweza.

Hata hivyo bado mguu wake wa kushoto ulikuwa umefungwa kwa plasta na bado alikuwa na mikongojo ya kumsaidia kusimama na kutembea.

Jalang'o alifanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kushoto baada ya kuumia alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya Bunge ya Mpira wa Kikapu mwishoni mwa mwezi Septemba.Aliruhusiwa kuenda nyumbani baada ya kulazwa katika Hospitali ya Nairobi kwa siku chache.

Baada ya kuruhusiwa kutoka, alifichua kuwa angesalia nyumbani ambapo angepitia safari yake ya wiki sita ya kupona.

"Ninataka kuchukua fursa hii kuwashukuru kila mtu kwa maombi yenu ya Kupona Haraka na ninyi nyote mlionitembelea katika Hospitali ya Nairobi," Jalang’o alisema kwenye Instagram mwishoni mwa mwezi Septemba.

Mwandani huyo wa rais Ruto aliambatanisha taarifa yake na picha iliyomuonyesha akiwa amejipumzika kwenye sofa nyumbani kwake huku mikongojo ya kumsaidia kutembea ikiwa kando. Mguu wake wa kushoto ambao ulijeruhiwa ulikuwa umefungwa ili kumsaidia kupona baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Ninataka kushukuru timu nzima ya hospitali ya Nairobi inayoongozwa na Prof. Atinga kwa kazi nzuri na ukarimu wao wa jumla na huduma. Tuko chini lakini hatujatoka! Timu yetu ya Langata yenye uwezo itasimamia masuala ya eneo bunge yakifuatiliwa kwa karibu na mimi mwenyewe. ASANTENI saana!” alisema.

Akizungumzia jeraha lake, alifichua kuwa alipata ajali alipokuwa akifanya mazoezi na timu ya mpira wa vikapu ya Bunge mnamo Jumanne, Septemba 26.

Ajali hiyo ilimsababishia jeraha kubwa kwenye mguu wa kushoto na kupelekea yeye kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha sehemu iliyoharibiwa baada ya uchunguzi wa MRI.

"Jumanne iliyopita wakati wa mazoezi yetu ya asubuhi ya mpira wa kikapu ya Bunge nilipata ajali iliyorarua kano zangu, nilifanyiwa upasuaji wa kurekebisha na kurejea nyumbani wakati safari ya wiki 6 ya kupona inaanza," alisema.