Watu wenye alama ya D+ kwenye KCSE hawatapata nafasi ya kuajiriwa kuwa polisi nchini

Jopokazi lililobuniwa kuangazia mabadiliko katika idara ya polisi likiongozwa na aliyekuwa jaji mkuu David Maraga linapendekeza alama ya chini kabisa kuajiriwa kama polisi iwe C-

Muhtasari

• “Ili kutatua suala la kutokomaa kiakili ambalo limekuwa likionekana kwa makurutu wapya, umri wa chini unastahili kupandishwa kutoka miaka 18 hadi 21,” jopokazi hilo lilisema.

KDF kuajiri mwezi ujao,
KDF kuajiri mwezi ujao,
Image: Maktaba

Kikosi Kazi cha Kitaifa kuhusu Marekebisho ya Polisi kimetoa mapendekezo muhimu ya kuajiri maafisa wa siku zijazo katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi na Huduma ya Magereza ya Kenya.

Muhimu kati ya mapendekezo haya ni kwamba sifa za kitaaluma za wanaotaka kujiandikisha zipandishwe kutoka daraja la sasa la chini kabisa la KCSE la D plus hadi C minus.

Katika mapendekezo yake, jopokazi hilo linaloongozwa na jaji mkuu mstaafu David Maraga lilisema kuinua sifa za kuajiri kutaongeza weledi katika utumishi wenye nidhamu.

“Jopokazi hili linapendekeza kiwango cha chini cha mtu kuruhusiwa kuajiriwa katika idara ya polisi kupandishwa hadi C- kutoka  D+ katika mtihani wa KCSE,” sehemu ya taarifa hiyo ilisoma.

Hata hivyo, Maraga na wenzake katika pendekezo hilo ambalo waliwasilisha kwa rais mwishoni mwa juma, walipendekeza kuwa wale kutoka maeneo yanayohisi kutengwa wapewe nafasi ya kuingia jeshini ya alama ya D+

Kando na pendekezo hilo la kiwango cha alama, jopokazi hilo pia lilipendekeza muda wa kufunzwa kwa makurutu kuongezwac hadi miezi 12 kutoka kwa miezi 9 ya sasa.

Na pia walipendekeza umri wa chini kupandishwa kutoka miaka 18 hadi miaka 21 ili kusuluhisha suala la kutokomaa.

“Ili kutatua suala la kutokomaa kiakili ambalo limekuwa likionekana kwa makurutu wapya, umri wa chini unastahili kupandishwa kutoka miaka 18 hadi 21,” jopokazi hilo lilisema.