Wacha kunilaumu kwa mapungufu ya uongozi wako - Uhuru amwambia Ruto

"Kila wakati mtu anashindwa kufanya kazi yake, anaanza kulaumu uongozi uliopita, hata wakati mke wa mtu anashidnwa kushika mimba, wanamlaumu Uhuru,” alisema .

Muhtasari

• Alisisitiza kwamba kutupiwa lawama hakutabadili msimamo wake wa kuendelea kusimama na kutetea sera za mrengo wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga.

Ruto na Uhuru
Ruto na Uhuru
Image: Facebook

Kwa mara nyingine tena rais mstaafu Uhuru Kenyatta amemtaka rais William Ruto kukoma kumlimbikizia lawama kwa kile alisema ni mapugunfu ya uongozi wake.

Akizungumza katika ibada ya kanisa Jumapili kaunti ya Kitui, Kenyatta alisema kwamba uongozi wa sasa umeshinda kila mara ukimhusisha na mapungufu ambayo hahusiki kwani yeye alishakabidhi uongozi.

“Nisingependa kusema chochote lakini ili kimya changu kisichukuliwe kwamba mimi ni muoga wa kuzungumza kilichopo akilini mwangu, ni wazi sasa kwamba baadhi ya watu wamefeli katika kufanya kazi yao. Siku hizi nimezoea kuhusishwa kwa kila lawama. Kila wakati mtu anashindwa kufanya kazi yake, anaanza kulaumu uongozi uliopita, hata wakati mke wa mtu anashidnwa kushika mimba, wanamlaumu Uhuru,” alisema huko mwingi.

Itakumbukwa kwa Zaidi ya mwaka mmoja sasa tangu walipokabidhiwa uongozi, Ruto na naibu wake pamoja na mawaziri wengi wamekuwa wakitupa lawama kwa uongozi wa Uhuru Kenyatta kwa kile wanasema kwamba uongozi wa Kenyatta kwa kushirikiana na ‘kakake’ Raila Odinga walihujumu uchumi wa nchi.

Ruto amekuwa akisema kwamba ugumu wa maisha ambao taifa linapitia sasa hivi ni kutokana na mikopo mingi ambayo serikali iliyopita ilikopa na kuitumia kwa njia zisizo halali.

Jumapili Uhuru Kenyatta alifanya ziara ya kushtukiza katika kaunti ya Kitui ambapo alilakiwa na viongozi m,bali mbali wa Ukambani akiwepo Kalonzo Musyoka.

Alisisitiza kwamba kutupiwa lawama hakutabadili msimamo wake wa kuendelea kusimama na kutetea sera za mrengo wa upinzani ukiongozwa na Raila Odinga.