• Majirani waliitikia wito huo wa dhiki, na mara moja wakaarifu serikali ya Kaunti. Timu ya wazima moto ilitumwa mahali hapo.
Ajuza wa miaka 60 katika kaunti ya Kirinyaga alikuwa na bahati kama ya mtende baada ya kuokolewa kutoka shimo la choo lenye kina cha urefu wa futi 45 baada ya kuanguka humo ndani na kukaa kwa Zaidi ya nusu saa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Citizen, mama huyo ambaye ni mmiliki wa nyumba za kukodisha katika kaunti hiyo kwa jina Wangithi Koori alisikika akipiga usiahi kutoka ndani ya shimo la choo ndani ya boma hilo lake.
Majirani waliitikia wito huo wa dhiki, na mara moja wakaarifu serikali ya Kaunti. Timu ya wazima moto ilitumwa mahali hapo.
"Alikaa ndani ya choo hiki cha shimo kwa takriban dakika 30 tulipokuwa tukisubiri wazima moto kuwasili," jirani wa Wangithi Peter Mwangi alinukuliwa katika taarifa.
Wangithi amelazwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya, na jamaa wanasema anaendelea vyema na matibabu.
Wangithi ni mama mwenye nyumba, ambaye anapangisha nyumba zake kwa wanafunzi kadhaa katika Chuo Kikuu cha Kirinyaga.
"Hizi ni hosteli za wanafunzi wa chuo kikuu cha Kirinyaga na tunashangaa kwa nini anatumia choo cha zamani cha mabati ilhali ana uwezo wa kujenga choo bora katika boma hili," mmoja aliuliza.