Hazina ya kitaifa yatenga Sh1.1 bilioni kudhibiti saratani

Waziri Ndung'u amesema hii itasaidia kupunguza mzigo wa matibabu miongoni mwa wakenya

Muhtasari

•Jumla ya Ksh.1.1 bilioni zimetengwa na wizara ya fedha ili kudhibiti saratani.

•Ili kuboresha utoaji wa huduma za afya,waziri pia ametenga Sh29.7 bilioni zaidi kwa hospitali ya kitaifa ya Kenyatta na hospitali ya mafunzo ya Rufaa ya Moi.

Waziri wa fedha
Njuguna Ndung'u Waziri wa fedha
Image: the star

Hazina  ya kitaifa imetenga Ksh 1.1 bilioni katika mwaka wa fedha wa 2024/25 ili kudhibiti saratani.

Waziri wa fedha ,Njuguna Ndung'u alisema hii imetolewa ili kuimarisha utambuzi wa mapema na udhibiti wa saratani katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta (KNH) na hospitali ya Kisii Level 5.

Aidha alitoa kiasi cha Sh2 bilioni kwa ajili ya hazina ya dharura na magonjwa sugu na mahututi.  Ndung'u alisema kuwa hii itasaidia kupunguza mzigo wa matibabu miongoni mwa wakenya.

Vile vile, Ndung'u alisema ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ametenga Sh29.7 bilioni zaidi kwa Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi.

“Hii ni pamoja na Sh2.6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha watoto cha KNH, Sh5.2 bilioni za shirika la ugavi wa dawa la Kenya, Sh2.5 bilioni za taasisi ya utafiti wa matibabu ya Kenya, Sh1 bilioni kwa ununuzi wa bidhaa za uzazi wa mpango na Sh.760 milioni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa katika huduma ya taifa ya kuongeza damu,” Waziri wa fedha alisema.

Ili kuimarisha uwezo wa madaktari Ndung'u alipendekeza kutengewa Sh3.7 bilioni kwa wahudumu wa afya, Sh406 milioni kwa mafunzo ya wafanyikazi wa afya na Sh8.6 bilioni kwa kituo cha mafunzo ya matibabu cha Kenya.