Jalang’o asaliti urafiki wake na rais Ruto na kuupinga mswada wa fedha 2024 bungeni

“Wakati wengi wa wabunge watakaporudi vijijini kwenye maeneobunge yao, tutasalia hapa Nairobi na Gen Z. Wengi wenu mnajua mimi ni rafiki wa karibu wa rais, niizungumza naye na anajua vizuri kwamba huu ndio msimamo wangu,” Jalang’o alisema.

Muhtasari

• Mswada huo unatarajiwa kupigiwa kura majira ya saa tisa na nusu alasiri baada ya kusomwa rasmi na mbunge wa Molo Kimani Kuria ambaye pia ni mwenyekiti wa ripoti hiyo.

Image: HISANI// FACEBOOK

Katika kile ambacho kimekuja kama mshangao kwa baadhi wa wafuatiliaji wa karibu wa siasa, mbunge wa Lang’ata Phelix Odiwuor maarufu kama Jalang’o amekiri wazi wazi mbele ya bunge kwamba anaupinga mswada wa fedha wa 2024.

Mswada huo unatarajiwa kupigiwa kura majira ya saa tisa na nusu alasiri baada ya kusomwa rasmi na mbunge wa Molo Kimani Kuria ambaye pia ni mwenyekiti wa ripoti hiyo.

Jalang’o ambaye tangu mwaka jana amekuwa na ukaribu na rais Ruto licha ya kuwa kutoka mrengo wa upinzani kwa tikiti ya chama cha ODM alionekana kusaliti urafiki wake na Ruto na kusema kwamba atapiga kura ya kuukataa mswada huo.

Mbunge huyo alikiri kwamba ni rafiki wa Ruto lakini akafichua kwamba hata rais mwenyewe anajua msimamo wake utakuwa ni kuupinga.

Jalang’o alisema kwamba kinachomfanya kuupinga mswada huo ni kizazi cha Gen Z ambacho wengi wao wako Nairobi na ikiwa wataupitisha basi watasumbua sana jijini.

“Wakati wengi wa wabunge watakaporudi vijijini kwenye maeneobunge yao, tutasalia hapa Nairobi na Gen Z. Wengi wenu mnajua mimi ni rafiki wa karibu wa rais, niizungumza naye na anajua vizuri kwamba huu ndio msimamo wangu,” Jalang’o alisema.

Mbunge huyo mwaka jana alijikuta pabaya baada ya kuweka chini ya uchunguzi na kamati ya nidhamu ya ODM pamoja na wenzake 6 ambao walikwenda katika ikulu na kumtembelea rais Ruto mwishoni mwa mwaka 2022.

ODM waliwataja wabunge hao na seneta mmoja kama wasaliti ambao walikwenda inyume na msimamo wa chama.

Tangu wakati huo, Jalang’o amekuwa akionekana kuegemea Zaidi maamuzi na mapendekezo yanayopendekezwa bungeni na mrengo wa Kenya Kwanza, na safari hii imeonekana kuwa tofauti kwa kuwasaliti na kusimama na kile alisema ni sauti ya wananchi wapiga kura.