Mbunge Racheal Nyamai Akosoa Maandamano ya Gen Z

Mbunge huyo wa Kitui Kusini amedai wengi wa vijana wa Gen Z wanajihusisha kwa maandamano ili kupata umaarufu Tiktok

Muhtasari

•Racheal Nyamai amedai kuwa vijana wa Gen Z wanajihusisha tu kwa maandamano ili kupata umaarufu kwenye mtandao wa Tiktok.

•Hatma ya mswada wa fedha 2024 itafahamika leo Juni 20 baada ya wabunge kupiga kura.

Mbunge wa Kitui Kusini
Rachel Nyamai Mbunge wa Kitui Kusini
Image: Hisani

Mbunge wa Kitui Kusini Racheal Nyamai amedai kuwa maandamano ya vijana dhidi ya mswada wa fedha 2024 jijini Nairobi hayachochewi na nia nzuri, bali kupata tu umaarufu  Tiktok.

Nyamai alisema hayo alipokuwa akijadili muswada wa sheria ya fedha bungeni Jumatano Juni 19, 2024. Mbunge huyo alisema baada ya kushiriki maandamano hayo, mmoja wa wanafunzi anaowafadhili shuleni, alitoa maoni yake kwake.

Nyamai alidai kuwa mwanafunzi huyo alimtumia ujumbe mfupi wa simu kueleza wasiwasi wake kuhusu mswada wa fedha, haswa ushuru uliopendekezwa wa usambazaji wa chakula na magari.

Aidha, mbunge huyo alidokeza kuwa mwanafunzi wake aliyemfadhili hakuwa na sababu ya kuendelea kuandamana kwa sababu ushuru kwa upande wa chakula na magari ulikuwa umeondolewa.

"Nilimuuliza kwa nini alikuwa mtaani, na msichana akaniambia kuwa hayupo mtaani kuhusu mswada wa fedha, akaniambia alikuwa huko kwa sababu ya Tiktok..." Nyamai alisema.

Mbunge huyo pia aliendelea kutaja jinsi aliunga mkono mswada huo baada ya sheria ya fedha ya 2023 kufanikiwa. Pia alieleza kuwa sera za serikali zilizowekwa ziliwajibika kwa ukuaji wa uchumi wa Kenya.

Vile vile alidai kuwa kwa kutunga hatua zilizojumuishwa katika mswada wa fedha, ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ungehimiza ukuaji wa wazalishaji wa Kenya. Hii inakuja  baada ya vijana  kumiminika barabarani,wakitaka mswada wa fedha kutupiliwa mbali wengi wakidai kuwa ni kukandamiza wakenya.

Mswada wa fedha 2024,unazidi kupamba moto huku baadhi ya wabunge kama vile Robert Mbui kutoka Kathiani wakipinga,mbunge wa Mugirango Kusini,Silvanus Osoro akiunga mkono.

Hatma ya mswada wa fedha itabainika leo Juni 20 baada ya wabunge kupiga kura bungeni.