Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, mwanaharakati wa kisiasa na mwanamuziki wa Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu maarufu kama Bobi Wine amefichua kuwa anaunga mkono maandamano yanayoendelea nchini dhidi ya mswada Mswada wa Fedha.
Katika taarifa aliyochapishwa Jumapili, Juni 23, 2024, kupitia ukurasa wake rasmi wa mitandao ya kijamii, Bobi Wine aliwapongeza vijana wa Kenya kwa kujitokeza mitaani kutumia haki zao za kidemokrasia kutoa malalamiko yao.
Akielezea kufurahishwa kwake na waandamanaji wanaopinga mswada wa fedha, Bobi Wine alifichua kuwa sauti za waandamanaji zinasikika mbali Zaidi ya mipaka ya Kenya.
“Mnaongea na sauti zenu zinasikika mbali zaidi ya mipaka ya Kenya. Tunaendelea kusimama pamoja wakati mnapopingania haki zenyu.” Alisema.
Kiongozi huyo wa upinzani nchini Uganda, alisema kuwa ana matumaini sauti za waandamanaji zitasikizwa na serikali ya Kenya na kuongeza kuwa ataendelea kusimama kidete na waandamanaji wanaopinga mswada wa Fedha.
“Tunatumai viongozi pia wanasikiliza! Tunaendelea kusimama kwa mshikamano nanyi, nguvu kwenu vijana wa Kenya.” Alisema.