Mwanamitandao maarufu Shad Khalif atekwa nyara, alikuwa mmoja wa waliyopigia debe maandamano ya Gen-z

Shad Khalif alitekwa nyara Jumapili jioni eneo la South B,Nairobi na watu wasiojulikana.

Muhtasari

•Utekaji nyara huo ulifanyika Jumapili jioni na ni wa hivi punde zaidi kulenga wale wanaochukuliwa kuwa wanapinga mswada wa fedha wa 2024.

•Familia na marafiki wa Shad Khalif walisema hajulikani alipo baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana waliokuwa wamemfuata katika eneo hilo.

Shad Khalif
Image: Hisani

Shad Khalif,mmoja wa watu ambao wamekuwa wakipinga ushuru uliopendekezwa hayupo baada ya kutekwa nyara kutoka kituo cha biashara eneo la South B, Nairobi.

Utekaji nyara huo ulifanyika Jumapili jioni na ni wa hivi punde zaidi kulenga wale wanaochukuliwa kuwa wanapinga mswada wa fedha wa 2024.

Familia na marafiki wa Shad Khalif walisema hajulikani alipo baada ya kutekwa nyara na watu wasiojulikana waliokuwa wamemfuata katika eneo hilo. Gari nyeusi aina ya double-cab na Toyota Prado nyeupe zilionekana zikimfuata mtumiaji maarufu wa mitandao ya kijamii Shad Khalif kabla ya kutekwa nyara kwa nguvu katika eneo la South B, Nairobi Jumapili jioni na watu wanaoshukiwa kuwa wapelelezi waliovalia kiraia kwa kudhania kuwa yeye ni mkuu katika maandamano hayo.

Khalif amekuwa akipinga muswada huo kwa sauti kubwa. Hata alifanya mahojiano akielezea jinsi alivyojipata yeye na marafiki zake kwenye gari. Alisema hana mfadhili na kiongozi katika maandamano hayo .

Aidha,polisi hawakujibu maswali kuhusu tukio hilo. Kutekwa nyara kwake kulikuja saa chache baada ya daktari Dkt Austin Omondi ambaye pia alikuwa kwenye maandamano kutekwa nyara na kuachiliwa.

Maandamano ya kitaifa dhidi ya mswada wa sheria ya fedha wa 2024 yalivutia macho ya kimataifa wiki iliyopita huku wengi wakiunga mkono hatua ya kutupilia mbali mswada huo.

Maandamano hayo yanatazamiwa kuendelea wiki hii hadi kilele chake Alhamisi ambapo 'Gen Zs' wameonya kwamba watafunga barabara kuu zinazoelekea Nairobi na kuandamana hadi Ikulu.