Wajackoyah awaongoza wakenya nchini Marekani kupinga mswada wa fedha [Picha]

Wakenya huko Dallas walifanya maandamano kupinga mswada tata wa fedha ambao umezua wimbi la maandamano nchini.

Muhtasari

•Mswada huo, ambao umezua ghadhabu kubwa, umetajwa na wakosoaji kuwa unaathiri ustawi wa kiuchumi wa wakenya wa kawaida.

•Wajackoyah, anayejulikana kwa msimamo wake wazi kuhusu masuala mbalimbali ya kitaifa, alionyesha kuunga mkono jitihada ya kutaka mswada huo uangushwe.

George Wajackoya
Image: Facebook

Kiongozi wa chama cha Roots George Wajackoyah aliongoza wakenya katika kupinga mswada wa fedha wa 2024 huko Dallas, Marekani mnamo Juni 23,2024.

Wajackoyah, ambaye alikuwa mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 aliwashukuru vijana wa Kenya, hasa 'Gen-Z' kwa kuandaa maandamano ya amani kupinga mswada wa fedha.

Kwenye mazungumzo na wanahabari mjini Dallas,Marekani siku ya Jumapili, Wajackoyah alisisitiza kuwa mswada wa fedha  lazima ukataliwe na wakenya wote, wakiwemo viongozi walioteuliwa na hata kuweka  chapisho kwa ukurasa wake wa Facebook.

"Leo niliungana na wakenya huko Dallas Texas, Marekani kuandamana dhidi ya mswada mbaya wa fedha nchini Kenya," Wajakoya alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Kiongozi huyo wa chama cha Roots pia alitoa wito wa kuwepo kwa mshikamano miongoni mwa wakenya ndani na nje ya nchi, na kuwataka raia wa Kenya wanaoishi nje ya nchi kueleza wasiwasi wao na kuunga mkono maandamano ya  kupinga mswada wa fedha.

Matamshi yake yanaibuka wakati wakenya walipokuwa wakihamasishwa kwenye mitandao ya kijamii kuendelea na maandamano ya jijini Nairobi na maeneo mengine ya nchi wiki hii.

Vijana wengi wameapa kufunga njia zote za kuingia Nairobi na kufika hadi kwenye Ikulu.