logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Khalwale atupa lawama za masaibu ya rais Ruto kwa Gachagua, Mudavadi na Wetang’ula

Wakati Khalwale anawalaumu watatu hao, DP Gachagua naye ameilaumu NIS.

image
na Davis Ojiambo

Habari28 June 2024 - 10:19

Muhtasari


  • • Wakati Khalwale anawalaumu watatu hao, DP Gachagua naye ameilaumu NIS kwa kufeli kufanya kazi, haswa mkuu wake, Noordin Hajji.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale amewalaumu baadhi ya viongozi wakuu kwenye baraza la mawaziri la rais Ruto kwa kushindwa kumshauri rais mapema kuhusu mswada tata wa kifedha wa mwaka 2024.

Kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X, kiranja huyo wa walio wengi katika seneti alisema naibu wa rais Rigathi Gachagua, mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi na spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula ndio walifeli katika kumshauri rais kuhusu mori ya wananchi.

Kwa mujibu wa Khalwale, kama watatu hao wangemshauri dhidi ya mswada huo ambao ulivutia pingamizi kali kutoka kwa umma, machafuko yaliyotokea hayangetokea na maafa yangezuiliwa.

“Naibu Rais, Mh. Riggy G, PCS Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge Moses Wetangula, viongozi waliokomaa na wenye tajriba karibu na Rais William Ruto walishindwa pakubwa kuhusu suala la Mswada wa Sheria ya Fedha wa 2024. Wangemshauri vinginevyo. Roho za wote waliopoteza maisha zipumzike kwa amani ya milele,” Khalwale alisema, akichapisha picha za watatu hao.

Mswada tata wa fedha wa 2024 ulizua mori na ghadhabu nyingi kutoka kwa Wakenya ambao licha ya kuwaonya wawakilishi wao bungeni dhidi ya kuupitisha, wabunge wengi walipiga kura ya ‘Yes’ kupelekea machafuko ya maandamano katika takribani kaunti 30 humu nchini.

Maandamano hayo yalianza kama mzaha wiki mbili zilizopita na kufululiza hadi kwenye kilele chake Jumanne wiki hii ambapo vijana waliokuwa na simu pekee bila silaha walivamia majengo ya bunge na kufaniiwa kuingia ndani kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa la Kenya.

Mtafaruku huo ulishuhudia machafuko mabaya kuwahi kutokea katika majengo ya bunge, ambapo vijana kadhaa waliuawa na polisi kwa kufyatuliwa risasi huku wengine wakiingia na kuharibu sehemu mbalimbali za majengo hayo.

Ghadhabu hii ilimfanya rais Ruto kuitisha mkutano wa ghafla wa wabunge wa mrengo wa serikali na kuafikiana kwa pamoja kuutupilia mbali mswada huo ambao ulikuwa umepitishwa na kumsubiria yeye kuutia saini ili kuwa sheria.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved