DCI yachapisha picha za wanaosakwa kuhusiana na maandamano

Watu hao wanadaiwa kuvuruga na kuharibu mali za umma wakati wa maandamano dhidi ya mswada wa fedha 2024

Muhtasari

•Idara ya upelelezi imetoa picha za washukiwa wanaosakwa baada ya kujihusisha katika shughui zisizo za halali wakati wa maandamano.

•Wananchi  wametakiwa kujitolea kutoa taarifa za mahali walipo watu hao kwa kuwasilisha maelezo  kwenye nambari ya simu 0800722203 au 999,911 au 112.

Idara ya upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) imetoa picha za washukiwa wanaosakwa wanaoaminika kupanga shughuli zisizo halali wakati wa maandamano ya kuipinga serikali.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye jukwaa la X, DCI ilitoa picha za watu wanaosakwa, ambao wameagizwa kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu kwa hatua zaidi za polisi.

"Watu ambao picha zao zinaonekana hapa chini wanasakwa na polisi kwa shughuli zao zisizo halali wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha.Kwa hivyo tunawashauri kuripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu kwa hatua zaidi za polisi," Chapisho la DCI lilisomeka.

Wananchi pia wametakiwa kujitolea kutoa taarifa za mahali walipo watu hao na wametakiwa kuwasilisha maelezo yao bila majina kwenye nambari ya simu 0800722203 au 999,911 au 112.

Haya yanajiri baada ya DCI kutoa onyo kali kwa watu waliopanga kutumia maandamano ya kitaifa dhidi ya serikali kama njia ya kutekeleza shughuli zao mbaya.

Maandamano ya amani ambayo yalikuwa yakifanyika kote nchini baadaye yaligeuzwa kuwa ghasia na wahuni. Wengi  wakijipenyeza katikati mwa jiji la Nairobi na sehemu mbalimbali za nchi kwa kujaribu kuharibu na kuiba kutoka kwa biashara mbalimbali.

Vijana wa Gen Z ,ambao hapo awali waliongoza maandamano haya walifanya alama ya amani na polisi na wafanyabiashara, hata hivyo, wahuni walibadilisha simulizi hii kupitia uporaji wa maduka mbalimbali na kuwarushia polisi mawe.

Baadhi ya waandamanaji walibaini mabadiliko katika anga wakisema kuwa tofauti na maandamano ya awali ya hivi karibuni zaidi yaliingiliwa na waasi ambao waliiba simu za watu na kuharibu biashara.

Kutokana na hali hiyo, waziri wa mambo ya ndani Kithure Kindiki, Jumanne alihakikishia umma kwamba wapangaji, watekelezaji na wafadhili wa uteketezaji mkubwa, wizi wa kutumia nguvu na uhalifu mwingine mbaya watafikishwa mahakamani.

“Enzi hii ya ugaidi dhidi ya watu wa Kenya na kutoadhibiwa kwa magenge hatari ya wahalifu lazima imalizike kwa gharama yoyote ile. Serikali imedhamiria kukomesha wahalifu wanaodai kutisha umma na kudhuru Kenya, licha ya majaribio ya kuingiza uhalifu kisiasa,” Kindiki alisema.