Jamaa asakwa na polisi baada ya kupeana bastola kanisani wakati wa kutubu

Polisi wanaamini kuwa mwanamume huyo alitaka kusalimisha silaha hiyo lakini hakuwa na uhakika wa kufanya hivyo na wapi.

Muhtasari

•Kisa hicho kilitokea Jumapili, Julai 7 alasiri katika kituo cha Instant Miracle ndani ya vitongoji duni vya Mukuru Kwa Njenga, Nairobi. 

•Mchungaji  aliwataka waumini kusimama na kutubu dhambi zao.

Picha ya bastola aina ya Ceska
Picha ya bastola aina ya Ceska
Image: MUSEMBI NZENGU

Polisi wanamtafuta mwanamume aliyeacha bastola kwenye mimbari ya kanisa alikokwenda kwa ajili ya toba katika tukio la kushangaza.

Kisa hicho kilitokea Jumapili, Julai 7 alasiri katika kituo cha Instant Miracle ndani ya vitongoji duni vya Mukuru Kwa Njenga, Nairobi.

Kulingana na polisi, mwanamume huyo mwenye umri wa makamo aliweka bastola yake kwenye mimbari alipokuwa akienda kutubu huku waumini wengine wakionekana kushtuka.

Viongozi watatu wa kanisa waliripoti kuwa walikuwa wakiendesha ibada katika kituo hicho na ulikuwa wakati wa toba. Walisema ,mchungaji  aliwataka waumini kusimama na kutubu dhambi zao.

Hapo ndipo mmoja wa wale waliosimama na kwenda kwenye mimbari akachomoa bunduki kutoka eneo la kiuno chake na kuiweka juu ya meza.

Kisha mtu huyo aliondoka  katika eneo, huku wale wengine ambao pia walikuwa wamesimama kutubu wakitoroka kwa usalama bila kujua ni nini kilikuwa kinaendelea.

Silaha hiyo iliwekwa kabla ya  polisi kuitwa kwenye eneo la tukio na kuthibitisha kuwa ni kweli. Kulingana na polisi, bastola hiyo ilikuwa bastola ya Colt Double Action 45. Hata hivyo haikuwa na marisasi.

Polisi walisema sasa wanamsaka mtu aliyehusika na kusalimisha silaha hiyo.Pia wanataka kubaini ikiwa silaha hiyo imetumika mahali popote kufanya uhalifu. Aidha ,walitaka pia kujua mtu huyo aliipata wapi silaha hiyo.

Silaha hiyo ilichukuliwa kwa majaribio ya balestiki huku msako wa mtu aliyekuwa na bunduki ukiendelea.

Polisi wanaamini kuwa mwanamume huyo alitaka kusalimisha silaha hiyo lakini hakuwa na uhakika wa kufanya hivyo na wapi.