KPLC yatangaza maeneo yatakayoathirika na kukatizwa kwa umeme leo, Jumatatu

Kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanywa kwenye mitambo.

Muhtasari

•Baadhi ya maeneo ya kaunti nne za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili unusu asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Kenya Power
Image: HISANI

KAMPUNI ya kusambaza umeme nchini Kenya (KPLC) imeonya kuhusu kukatizwa kwa umeme katika maeneo kadhaa nchini siku ya Jumatatu, Julai 8. 

Katika taarifa ya Jumapili jioni, kampuni hiyo ilisema kukatizwa kwa umeme kutatokana na ukarabati ambao utakuwa ukifanywa kwenye mitambo.

Walisema baadhi ya maeneo ya kaunti nne za Kenya yatakosa umeme kati ya saa mbili unusu asubuhi na saa kumi na moja jioni. Kaunti ambazo zitaathirika ni pamoja na  Nairobi, Narok, Tharaka Nithi, na Embu.

Katika kaunti ya Nairobi, sehemu kadhaa za mtaa wa Kitsuru zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Sehemu kadhaa za eneo la Oldonyorok katika kaunti ya Narok zitakosa umeme kati ya saa tatu asubuhi na saa tisa alasiri.

Baadhi ya sehemu za eneo la Gituaka katika kaunti ya Tharaka Nithi zitaathirika na kukatizwa kwa umeme kati ya saa mbili unusu asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Katika kaunti ya Embu, sehemu za eneo la Kathangari pia zitakosa umeme kati ya saa mbili unusu asubuhi na saa kumi unusu jioni.