“Nilianza kumuunga mkono Raila Odinga 2005, sasa imefika mwisho!” – wakili Donald Kipkorir

“Sasa kwa vile Baba hakuweza kutuongoza na Gen Z bila Kiongozi wamechukua usukani, inanihuzunisha kwamba Baba anataka kuharibu wakati huu wa mabadiliko. Kati ya Gen Z na Raila Odinga, nachagua Gen Z.”

Muhtasari

• Wakili huyo pia aliwasifia vijana wa Gen Z kwa kuonyesha taifa kwamba nchi bila misingi ya kikabila ni jambo linaloweza kufanyika.

WAKILI KIPKORIR AMTEMA ODINGA
WAKILI KIPKORIR AMTEMA ODINGA
Image: MAKTABA

Wakili Donald Kipkorir ameeleza kusitisha kumuunga kinara wa upinzani na chama cha ODM, Raila Odinga.

Kupitia ukurasa wake wa jukwaa la X, Kipkorir alieleza kwamba alianza kumuunga Odinga mkono mwaka 2005 lakini sasa imefika mwisho na amewakumbatia Gen Z ambao wameonekana kuwa na makali zaidi ya kuikomboa Kenya kuliko Odinga ambaye juhudi zake kwa miongo kadhaa zimekuwa zikifeli.

Wakili huyo pia alionyesha kusikitishwa kwake kwa kile alikitaja kwamba Odinga ndiye sasa ameonekana kutumika kupiga breki mageuzi ya kisiasa ambaye yamefanikishwa na vijana wa Gen Z ndani ya kipindi kifupi cha maandamano yao ya Amani.

“Sasa kwa vile Baba hakuweza kutuongoza na Gen Z bila Kiongozi wamechukua usukani, inanihuzunisha kwamba Baba anataka kuharibu wakati huu wa mabadiliko. Kati ya Gen Z na Raila Odinga, nachagua Gen Z.”

“Kwa heshima kubwa kwa mchango wake hadi sasa katika demokrasia yetu, ninahitimisha uungaji mkono wangu kwa Baba ulioanza mwaka wa 2005. Natumai na ninaomba Gen Z watatuongoza hadi Kanaani katika maisha yangu. . UAMINIFU WANGU KWA RAILA ODINGA UMEISHIA LEO,” alichapisha.

Wakili huyo pia aliwasifia vijana wa Gen Z kwa kuonyesha taifa kwamba nchi bila misingi ya kikabila ni jambo linaloweza kufanyika.

“Gen Z wamenipa matumaini kuwa Kenya bila UTABIRI, UFISADI, UZALENDO na CRONYISM inawezekana. Kenya ambayo inathamini watoto wake wote zaidi ya KABILA, CREED, DARASA, JINSIA & UMRI. Kenya bila vurugu za kisiasa. Kenya ambayo Polisi HAWAUI au KUTEKA NYARA. Kenya ambayo huhitaji kuhonga ili kupata zabuni kutoka kwa Serikali au rushwa ili kulipwa kwa bili ambazo hazijalipwa. Ilikuwa ni Kenya ambayo kwa muda mrefu niliamini ni KANAANI ambayo Baba Raila Odinga atatuongoza” alisema.