USA yavunja kimya kuhusu utekaji nyara na kupigwa risasi kwa wanahabari na waandamanaji Kenya

Ubalozi wa Marekani ulitoa taarifa, ukisikitikia jinsi serikali ya Ruto na maafisa wake wa polisi wamekuwa wakiwaua kwa kuwapiga risasi waandamanaji pamoja na kuwajeruhi waandishi wa habari.

Muhtasari

• “Tunasikitika pakubwa kuhusu visa vya vita, ikiwemo mashambulizi ya risasi na utekaji nyara dhidi ya waandamanaji, waandishi wa habari na wengine,” sehemu ya ripoti yao ilisoma.

Serikali ya Marekani kupitia ubalozi wake nchini Kenya wamevunja kimya chao kuhusu vurugu na visa vya utovu wa usalama vinavyoshuhudiwa nchini Kenya kufuatia maandamano ya vijana ambayo yamedumu kwa mwezi sasa.

Kupitia ukurasa wa jukwaa la X, ubalozi wa Marekani ulitoa taarifa, ukisikitikia jinsi serikali ya Ruto na maafisa wake wa polisi wamekuwa wakiwaua kwa kuwapiga risasi waandamanaji pamoja na kuwajeruhi waandishi wa habari.

“Tukiwa tumeingia wiki ya 5 ya maandamano kote nchini Kenya na kuvuka idadi ya vifo 50 kutokana na maandamano hayo, ubalozi wa Marekani unaeleza kwa mafadhaiko makubwa kupotea kwa maisha na riziki za watu na kuwaomba washirika wote kuwa watulivu na kufuata sheria.”

“Tunasikitika pakubwa kuhusu visa vya vita, ikiwemo mashambulizi ya risasi na utekaji nyara dhidi ya waandamanaji, waandishi wa habari na wengine,” sehemu ya ripoti yao ilisoma.

Ubalozi huo pia uliwataka maafisa wa polisi kuwa watulivu ili kuwapa watu haki yao ya kikatiba kuandamana kwa njia ya Amani huku pia wakiwataka wanaochochea vurugu katika maandamano ya Amani kukoma kujihushisha na maandamano hayo.