Musalia Mudavadi amekanusha madai ya kuwepo njama ya serikali kuuza JKIA (video)

“Wacha ninyooshe maelezo mara moja kwamba uwanja wa ndege JKIA si wa kuuzwa. Hii ni mali ya umma, ni mali ya kimkakati" alisema.

Muhtasari

• Akizungumza alipofika mbele ya bunge kujibu madai hayo, Mudavadi alisema kwamba huo ni uvumi na JKIA haiuzwi kamwe na serikali.

PCA MUDAVADI
PCA MUDAVADI
Image: FACEBOOK

Waziri mwenye mamlaka makuu serikalini Musalia Mudavadi amekanusha madai kwamba kuna njama ya serikali ya William Ruto kuuza uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kwa kampuni ya Kihindi.

Akizungumza alipofika mbele ya bunge kujibu madai hayo, Mudavadi alisema kwamba huo ni uvumi na JKIA haiuzwi kamwe na serikali.

“Wacha ninyooshe maelezo mara moja kwamba uwanja wa ndege JKIA si wa kuuzwa. Hii ni mali ya umma, ni mali ya kimkakati na kama ilikuwa inakwenda kuuzwa, itafanyika hivyo tu baada ya mchakato mzima wa kushirikisha umma ambao bunge litaidhinisha,” Mudavadi alisema.

“Kwa hivyo yeyote anayezua dhana kwamba JKIA imeuzwa, huyo si mkweli na huo ni uongo.” Aliongeza.

Waziri huyo ambaye kwa sasa ndiye anashikilia majukumu yote katika baraza la mawaziri baada ya kuvunjwa kwa baraza lote la rais Ruto wiki mbili zilizopita hata hivyo alisema kwamba kuna haja kwa taifa kutambua kwamba ipo haja kubwa ya kufanya maboresho ya kisasa katika asasi hiyo ya kitaifa.

“Tunachostahili kukubaliana nacho ni kwamba tutahitaji kuboresha upya uwanja wetu wa ndege. Tunahitaji kituo kipya.”

Siku chache zilizopita, kuliibuliwa madai na baadhi ya wanasiasa kwamba kulikuwa na njama ya kupeanwa kwa haki za usimamizi wa JKIA kwa kampuni ya Kihindi.

Hili liliwafanya Wakenya wengi kuibua wasiwasi wao na hata kutangaza katika mitandao ya kijamii kwamba kungekuwa na maandamano ya kufurika katika uwanja huo kudai uwazi kuhusu dili hiyo.

Maandamano hayo kuelekea JKIA yaliratibiwa kufanyika leo Jumanne, lakini usiku wa kuamkia leo, maafisa wa polisi kutoka vitengo mbalimbali walikesha katika asasi hiyo kwa hofu kwamba waandamanaji wangeingia na kuzua rabsha.