Mbunge mteule John Mbadi amesema kuwa uteuzi wake kwa baraza la mawaziri ulikuja kwa mshangao.
Katika taarifa muda mfupi baada ya Rais William Ruto kumteua kama waziri wa hazina ya fedha ,Mbadi alitoa shukrani kwa Rais akisema kitendo hicho kilimshangaza.
"Kwa kweli uteuzi umekuja kama mshangao. Lakini zaidi ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi aliyonijalia,” alisema.
Mawaziri 10 walioteuliwa leo Julai 23,2024, sasa wamefika jumla ya mawaziri 20 hii ni baada ya uteuzi wa kwanza kufanyika Julai 19.
Mbadi, mshirika wa kinara wa ODM Raila Odinga, aliteuliwa katika kundi la pili la walioteuliwa pamoja na washirika wengine wa Raila .Opiyo Wandayi alikabidhiwa hati ya Nishati huku aliyekuwa gavana wa Mombasa Hassan Joho akiteuliwa kuwa waziri mteule wa Madini.
Ruto pia aliwateua tena washirika wake kwenye baraza la mawaziri. Aliyekuwa waziri wa uchukuzi na barabara Kipchumba Murkomen akipewa wizara ya vijana na michezo, Justin Muturi (Utumishi wa Umma), Salim Mvurya (Biashara) na Alfred Mutua (Kazi).
Mbadi alisema safu hiyo sio tu alama muhimu kuelekea umoja wa kitaifa lakini pia inadhihirisha kuwa maono ya Ruto kwa Kenya yanavuka misingi ya vyama vya siasa na maslahi ya kikabila.
"Naomba pia nimshukuru kwa dhati waziri mkuu wa zamani Mhe.Raila Odinga kwa imani yake isiyoyumba kwangu kwa miaka mingi na ninawaahidi watu wa Kenya sitakatisha tamaa katika azma ya serikali ya utoaji huduma bora na bora," Mbadi alisema.
Mbunge huyo wa kuteuliwa alisema akisubiri kuhakikiwa na kuidhinishwa na Bunge, anatarajia kushirikiana kikamilifu na rais na baraza la mawaziri katika kufufua uchumi.
"Kwa kweli, ninafahamu sana kazi niliyopewa si kazi ya kibabe, hasa wakati huu nchi inakabiliwa na changamoto kubwa za kiuchumi," alisema.