Katibu mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna ameshikilia kuwa chama chao hakijajiunga na serikali ya Rais William Ruto.
Kwenye mazungumzo na runinga ya Citizen,Sifuna alisema hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa na chombo chochote cha chama kilichoidhinisha kujiunga kwa serikali ya rais Ruto.
“Kama katibu mkuu nakaa katika vyombo vyote vya chama na mimi ndiye msemaji wa vyombo vyote hivyo, Wakenya wanataka tu mtu awaambie ukweli na kumekuwa na minong’ono mingi kuhusu umuhimu wa kilichotokea jana," Sifuna alisema.
"Ukweli wa mambo ni kwamba hakuna uamuzi wa chombo chochote cha ODM ambacho nitakaa kujiunga na serikali ya Ruto."
Aliendelea kusema kuwa kumekuwa na juhudi za kimakusudi za kukipaka chama cha ODM sura mbaya tangu kinara wa chama Raila Odinga alipohudhuria kutia saini mswada wa IEBC kuwa sheria katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Kenyatta (KICC).
Sifuna alishutumu vyombo vya habari kwa kupotosha msimamo wa chama hicho kuhusu suala hilo.
"Nadhani kumekuwa na juhudi za makusudi za kupotosha msimamo wa chama, haswa katika vyombo vya habari," aliongeza.
"Sijafurahishwa na jinsi vyombo vya habari vimechagua kuripoti mambo ambayo yametokea katika wiki chache zilizopita."
Alisema chama cha ODM huitisha tu mazungumzo ya kitaifa lakini hilo limegeuzwa kumaanisha mazungumzo kati ya ODM na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA).
Matamshi yake yanakuja baada ya rais Ruto kuwateua naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, mwenyekiti John Mbadi na kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa Opiyo Wandayi kujiunga na baraza lake la mawaziri.