Tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) imemkamata aliyekuwa mbunge Kutoka Kaskazini Mashariki na mkewe.
Inadaiwa kuwa mwanasiasa huyo aliwafyatulia risasi makachero wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi (EACC) waliokuwa wameenda nyumbani kwake katika msako uliomlenga mkewe.
Katika taarifa ya EACC, mkewe alikuwa mshukiwa mkuu wa sakata ya mamilioni ya fedha katika shirika la a kitaifa wa bima ya afya (NHIF).
Mbunge huyo wa zamani aliwafyatulia risasi maafisa wa upelelezi wa EACC walipokuwa wakijaribu kuingia nyumbani kwake, lakini hatimaye alikamatwa pamoja na mkewe.
"Wanandoa hao walikamatwa Alhamisi alasiri baada ya mbunge huyo kudaiwa kuwafyatulia risasi maafisa wa upelelezi wa EACC waliokuwa wameenda nyumbani kwake kwa ajili ya msako unaomlenga mkewe, mshukiwa mkuu wa sakata ya mamilioni ya NHIF inayochunguzwa na tume," EACC ilisema.
Upekuzi katika nyumba hiyo ulifanikisha kupatikana kwa mabegi yaliyokuwa na Dola za Marekani bandia zinazokadiriwa kuwa na thamani ya mamilioni ya fedha pamoja na kemikali mbalimbali.
"Wakati wa operesheni hiyo, wapelelezi walipata mikoba miwili iliyojaa dola za Kimarekani, zinazokadiriwa kuwa mamilioni, na kemikali mbalimbali (zikiwa za unga na kioevu) zinazoshukiwa kutumika kutengeneza noti bandia. Sampuli za noti zilizojaribiwa katika taasisi ya uchunguzi ya kifedha ya EACC. Maabara zilikuwa ghushi," EACC iliongeza.
Mbunge huyo wa zamani na mkewe walikabidhiwa kwa kurugenzi ya upelelezi wa makosa ya Jinai (DCI) pamoja na vitu vilivyopatikana na bastola aina ya Ceska yenye leseni iliyoisha muda wake.
Kulingana na EACC, oparesheni hiyo ililenga washukiwa saba, akiwemo mke wa mbunge huyo, meneja wa NHIF tawi la Eastleigh na wakurugenzi watano wa duka la dawa la Beirut Pharmacy, ambao kwa njia ya ulaghai walijipatia Sh199 milioni kutoka NHIF kupitia madai ya uwongo yaliyowezeshwa na maafisa wa NHIF.