FIDA wameipa idara ya polisi siku 3 kumkamata Collins Jumaisi na kumwasilisha kortini

Jumaisi, mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 ambao vipande vya miili yao vilipatikana vimetupwa katika timbo la taka chafu huko Kware Embakasi alitoroka kutoka seli katika kituo cha polisi cha Gigiri.

Muhtasari

• Kupitia ukurasa wao wa X, FIDA-Kenya walisema kwamba walipata ujumbe wa Jumaisi kutoroka seli kwa mshtuko mkubwa.

ambaye anashukiwa kuua wanawake kadhaa na kutupa miili yao katika eneo la kutupa taka la Kware, Mukuru kwa Njenga.
Collins Jumaisi ambaye anashukiwa kuua wanawake kadhaa na kutupa miili yao katika eneo la kutupa taka la Kware, Mukuru kwa Njenga.
Image: HISANI

Shirikisho la wanasheria wa kike nchini Kenya, FIDA limetoa makataa ya siku 3 kwa idara ya polisi kumkamata mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 na kutupa vipande vya miili yao katika timbo la Kware, Embakasi, Collins Jumaisi Khalusha.

Kupitia ukurasa wao wa X, FIDA-Kenya walisema kwamba walipata ujumbe wa Jumaisi kutoroka seli kwa mshtuko mkubwa.

Walisema kwamba idara ya polisi ina siku 3 pekee kuhakikisha Jumaisi ametiwa mbaroni tena na si tu kuzuiliwa katika seli bali kuwasilishwa mahakamani ili familia za wanawake waliouawa na miili yao kutupwa timboni Kware kupata haki.

“FIDA-Kenya ina wasiwasi mkubwa kutokana na kutoroka kwa mshukiwa wa mauaji ya Kware Collins Jumaisi kutoka kwa polisi wa Gigiri. Tunaomba polisi wamshike tena mshukiwa mara moja ndani ya siku tatu zijazo na kuendelea kumshtaki katika mahakama ya sheria,” walisema.

FIDA-Kenya walienda mbele kutishia kwamba kama makataa haya hayatafanikishwa, wataandaa maandamano ya nchi nzima kueleza kutoridhishwa kwao kwa jinsi Jumaisi alitoroka seli kwa njia tatanishi.

“Ikiwa hili halitafanikishwa, tutaandaa maandamano ya nchi nzima kuelezea mafadhiko yetu na kutaka uwajibikaji. Usalama wa jamii yetu, wanawake na watoto hauwezi kuathiriwa na tunahimiza vyombo vyote vinavyohusika kuchukua hatua haraka na kwa uamuzi,” ripoti yao ilisoma zaidi.

Jumaisi, mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake 42 ambao vipande vya miili yao vilipatikana vimetupwa katika timbo la taka chafu huko Kware Embakasi alitoroka kutoka seli katika kituo cha polisi cha Gigiri.