“Naamini Mungu atanifanya niwe rais wa 6 wa Kenya” – Moses Kuria

"Mimi ni muumini. Ninaamini kabisa kuwa atanifanya kuwa kiongozi na msemaji wa sasa wa Mlima Kenya na Rais wa 6 wa Jamhuri ya Kenya. Asante Ndugu,” Kuria alisema.

Muhtasari

• Itakumbukwa wawili hao walikuwa wanatupiana maneno wakati wote walikuwa kwenye baraza moja la mawaziri chini ya rais William Ruto.

Waziri Kuria Aomba Radhi kwa matamshi yake
MAANDAMANO Waziri Kuria Aomba Radhi kwa matamshi yake
Image: Twitter

Aliyekuwa waziri, Moses Kuria amezua minong’ono ya kisiasa baada ya kudai kwamba ana Imani Mungu atamfanya kuwa mrithi wa rais William Ruto kama rais wa Kenya ajaye.

Kupitia X, Kuria alichapisha ujumbe wa kumjibu naibu rais Rigathi Gachagua aliyelenga kumshauri kutokata tamaa baada ya kuvuliwa wadhifa wa uwaziri katika mabadiliko ya Julai 11.

Rigathi Gachagua alimshauri Moses Kuria kuwa yeye bado ni mdogo kisiasa na hivyo hafai kusononeka kwa kutorejeshwa kwenye baraza jipya la mawaziri, akisema kuwa Mungu ndiye anajua.

“Kwa ndugu yangu Moses Kuria, tulia. Mungu hafungi mlango bila kufungua mwingine. Usikwame katika hilo kwa sana. Wakati muda mwafaka utafika, Mungu atakupa fursa zingine, wewe bado ni kijana mdogo,” Gachagua alimshauri Kuria.

Kwa pande wake, Kuria alimjibu akimshukuru kwa maneno hayo ya busara na kufichua kwamba mimani yake kubwa inamtuma kuamini kuwa Mungu atamfanya kuwa kiongozi na msemaji wa eneo pana la Mlima Kenya lakini pia rais wa 6 wa Kenya.

“Kwa ndugu yangu DP Rigathi Gachagua. Asante kwa maneno yako mazuri. Hakika Mungu ana mipango yake. Mimi ni muumini. Ninaamini kabisa kuwa atanifanya kuwa kiongozi na msemaji wa sasa wa Mlima Kenya na Rais wa 6 wa Jamhuri ya Kenya. Asante Ndugu,” Kuria alimjibu Gachagua.

Itakumbukwa wawili hao walikuwa wanatupiana maneno wakati wote walikuwa kwenye baraza moja la mawaziri chini ya rais William Ruto.

Hata hivyo, kutokana na shinikizo la maandamano ya vijana wa Gen Z, rais Ruto alilazimika kuvunja baraza lote la mawaziri na kusalia na waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi na naibu wake Rigathi Gachagua pekee.

Wiki mbili baadae, Ruto alitangaza baraza jipya la mawaziri, na japo aliwarudisha baadhi ya waliokuwa kaitka baraza la mawaziri la zamani, aliwatema nje Moses Kuria, Florence Bore, Ababu Namwamba miongoni mwa wengine.