Kitu ninchojutia zaidi ni zile siku 58 za mgomo wa madaktari – Susan Nakhumincha

"Hata wakati unafikiria kwamba unafanya vizuri, mnakumbuka sheria ya matokeo yasiyotarajiwa, kwamba umepanga kufanya vizuri lakini unaishia kwa hali kama hiyo,’ Nakhumincha alisema.

NAKHUMINCHA
NAKHUMINCHA
Image: HISANI

Aliyekuwa waziri wa afya, Susan Nakhumincha amefichua kwamba anajuta sana mgomo wa madaktari uliodumu kwa karibia miezi miwili wakati akiwa kama waziri miezi michache iliyopita.

Akizungumza Alhamisi wakati wa kumkabidhi vifaa vya kazi mrithi wake, Debra Barasa katika wizara hiyo, Nakhumincha alisema kwamba mgomo huo haungefaa kudumu kwa siku nyingi hivyo kwani uligharimu maisha ya wengi kutokana na kutokuwepo kwa madaktari kazini.

Mgomo huo ulidumu hadi siku 58.

“Kuna mambo ambayo pengine tungefanya vizuri chini ya mazingira ila ningependa kuchukulia kama ni moja kati ya safari ya hii kazi. Hata wakati unafikiria kwamba unafanya vizuri, mnakumbuka sheria ya matokeo yasiyotarajiwa, kwamba umepanga kufanya vizuri lakini unaishia kwa hali kama hiyo,’ Nakhumincha alisema.

“Kwa mfano mimi najuta sana wakati ambapo madaktari walikuwa kwenye mgomo, ulikuwa ni wakati mgumu sana kwetu sisi kama wizara,” aliongeza.

Nakhumicha alimwambia Barasa angepatikana kwake ikiwa angehitaji msaada au ushauri wake.

“Sijafika hapa kwa muda wa kutosha kumshauri dada yangu lakini naweza kusema hakuna maandishi ya jinsi unavyofanya mambo yako. Kuna Katiba, Sheria ya Afya na sera za wizara. Unapofanya kazi ndani ya vigezo, unapaswa kuwa na uwezo wa kusogeza,” alisema.

Barasa ana tajriba ya zaidi ya miaka 18 katika sekta ya afya na mipango ya afya.