Kenya Power wavunja kimya kupotea kwa umeme usiku wa Ijumaa maeneo mengi nchini

Hii ni mara ya kwanza nguvu za umeme kupotea chini ya waziri mpya, Opiyo Wandayi, zikiwa zimesalia chini ya saa 24 kabla ya kampeni ya 'Update token meter' kukamilika rasmi.

Muhtasari

• Kampeni hiyo iliyoanzishwa miezi miwili iliyopita inakamilika mwisho wa mwezi huu wa Agosti, ambao unakamilika chini ya saa 12 zijazo.

KENYA POWER
KENYA POWER
Image: FACEBOOK

Shirika la kusambaza nguvu za umeme nchini, Kenya Power limevunja kimya chake baada ya maeneo mengi humu nchini kushuhudia kupotea kwa umeme kwa saa kadhaa usiku wa Ijumaa.

Katika taarifa, kampuni ya shirika hilo imekiri kuwepo kwa usumbufu huo na kuwahakikishia wananchi kuwa juhudi zilifanyika haraka kurejesha umeme haraka iwezekanavyo.

"Tumepoteza usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ya nchi isipokuwa eneo la North Rift na sehemu za eneo la Magharibi," KPLC ilisema.

Kampuni hiyo ilionyesha masikitiko yake juu ya usumbufu uliojitokeza na kuomba uvumilivu kutoka kwa wateja wake.

 "Tunasikitika kwa usumbufu wowote uliojitokeza na tunawaomba wawe na subira kutoka kwa wateja wetu tunapofanya kazi ya kurejesha hali ya kawaida haraka iwezekanavyo. Tutatoa taarifa kuhusu maendeleo ya zoezi la kurejesha umeme haraka iwezekanavyo," iliongeza taarifa hiyo.

Hali hii inajiri zikiwa zimesalia saa chache tu kabla ya kampeni ya ku update token meter kukamilika.

Kampeni hiyo iliyoanzishwa miezi miwili iliyopita inakamilika mwisho wa mwezi huu wa Agosti, ambao unakamilika chini ya saa 12 zijazo.

Itakumbukwa pia hii ndio mara ya kwanza umeme umepotea katika maeneo mengi nchini, tangu waziri mpya wa nishati na kawi, Opiyo Wandayi kuchukua mamlaka kutoka kwa Davis Chirchir katika wizara hiyo.