• "Nimetoa ahadi kwamba nikimaliza ziara yangu ikiwa ni jukumu la rais nitarudi kuwa mwinjilisti kwa sababu huo ndio wito wangu wa asili,” alisema.
Rais William Ruto kwa mara ya kwanza ametoa sababu kwa nini anapenda kuzungumza na umati wa watu kutoka juu ya gari lake.
Akizungumza katika kaunti ya Bungoma, rais Ruto alisema kwamba kwa muda mrefu alifanya kazi ya kueneza injili kwa watu wengi kama mwinjilisti.
Alisema kwamba yeye alizoea kusimama katika maeneo ya juu kutangaza neno na jambo hilo lilimuingia hadi wakati alijikuta kwenye siasa.
Kiongozi wa taifa alisema kutokana na kuzoea kusimama maeneo ya juu kueneza injili kama mwinjilisti kwa watu, huwa amezoea kusimama juu ya gari lake anapohutubia watu.
"Mimi ni mwinjilisti na watu wengi wanashangaa kwa nini wakati mwingine nasimama sehemu zilizoinuka, wakati mwingine juu ya gari kwa sababu wakati mwelekeo wako ni mwinjilisti unakuwa na tabia ya mwinjilisti hata unapokuwa unafanya mambo mengine,” alisema.
Mkuu wa nchi aliweka wazi kwamba pindi atakapomaliza hatamu yake ya uongozi, atarejea kwenye kueneza injili kama mwinjilisti.
"Nimetoa ahadi kwamba nikimaliza ziara yangu ikiwa ni jukumu la rais nitarudi kuwa mwinjilisti kwa sababu huo ndio wito wangu wa asili,” alisema.
Katika siku za hivi karibuni, rais amejipata chini ya shinikizo baadhi ya wakenya wakimsuta kwa kile wanahisi ameanza kampeni za mapema kwa kuzuru maeneo mbali mbali nchini na kuhutubia watu kutoka juu ya gari lake.