Mswada wapendekeza kuhalalishwa kwa pombe asili

Seneta Chimera alisema endapo mswada huo utafaulu wauzaji watapokezwa leseni ili kufanya kazi bila shaka.

Muhtasari

•Mswada wawasilishwa kwa bunge la seneti ili kuhalalisha pombe za kienyeji.

•Seneta Raphael Chimera alisema kuwa pombe za kienyeji ni zenye afya na zimeafikia ubora unaohitajika kuhalalishwa.

muratina
Image: hisani

Huenda hivi karibuni haitakuwa hatia kutumia baadhi ya pombe za kienyeji ikiwa mswada uliyowasilishwa katika seneti utaidhinishwa. 

Seneta maalum  Raphael Chimera amewasilisha mswada unaolenga kuhalalisha  utengezaji, uuzaji na unywaji wa pombe za kiasili.  seneta huyo amesema mswada huo ikiwa utaidhinishwa utainua maslahi ya watengenezaji wa pombe hizo vijijini. 

Seneta huyo ambaye analenga pakubwa kubadilisha sheria zilizoko za  kudhibiti vileo anataka serikali kudhibiti mauzo na uagizaji wa vileo kutoka nje ya Kenya na kukumbatia vinywaji vya kiasili vinavyotengenezwa hasa vya kienyeji. Aidha aliitaka serikali ya Kenya kuiga mtindo wa mataifa jirani na ambayo yameonekana kukumbatia utumizi wa pombe zao za kienyeji.

"kile ambacho tunasema ni kuwa,kumekuwepo na hulka ya Wakenya kunywa vileo kwa sababu ya kupunguza mawazo ,lakini tukisema wakenya kutumia vile vya kienyeji watakuwa wanakunywa ili kujiburudisha,". Chimera alisema.

Kwa sasa mswada huo umewasilishwa kwenye bunge la seneti na endapo utafaulu utakuwa ni wakati mwafaka kwa watengezaji wa vileo hivi vya vienyeji kupata mapato ambayo yatawakimu kimaisha kwani watakuwa na uhuru wa kufanya shughuli hiyo baada ya kupokezwa leseni.

"Tutakuwa na nafasi ya kuhakikisha kwamba kileo ambacho unachotumia ni salama hasa kwa afya yako na kimeafikiana viwango hitajika vya ubora kwa soko. Kwa sasa tunafaa kuanzisha vita dhidi ya pombe haramu ambazo zinanuia kutelekeza afya ya watumizi". Aliongeza seneta huyo.

Mswada huo umewatia tabasamu wagema na watumiaji  wa vinywaji hivi na kufurahikia hatua hiyo kwani watafaidi pakubwa endapo mswada huo utafaulu.