Kenya ina wanagainakolojia 700 pekee

Hospitali mbili pekee nchini zina vifaa vya kuchunguza maradhi ya Endometriosis katika wanawake.

Muhtasari

• Wabunge walionyesha kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na wizara ya afya.

• Dkt. Pukose alipendekezea bunge kuhakikisha kwamba kila kaunti ina vifaa vinavyohitajika na kutoa mafunzo kwa madaktari wa magonjwa ya wanawake.

Mbunge la Kenya
Mbunge la Kenya
Image: Handout

Mwenyekiti wa kamati ya afya katika bunge la kitaifa Dkt. Robert Pukose mnamo Alhamisi aliiambia bunge kuwa Kenya ina wanagainakolojia 700 kote nchini.

Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa barua iliyowasilishwa na wizara ya afya kwa kamati ya afya katika bunge la kitaifa tarehe 12 Agosti, 2024.

Dkt. Pukose  alisema hayo akiwasilisha majibu ya kamati anayosimamia kwa wabunge waliotaka kufahamu kuhusu hali ya ukosefu wa vifaa maalum vya kushughulikia wagonjwa wa Endometriosis.

Kamati hiyo ilibaini kuwa Kenya ina gainakolojia 700 kote nchini katika barua iliyowasilishwa na wizara ya afya kwa kamati inayoongozwa na Dkt. Pukose.

"Serikali imewekeza katika mafunzo ya gainakolojia. Sasa hivi, tumesajili wanagainakolojia 700 wanaofanya kazi  katika sehemu tofauti tofauti nchini katika sekta ya umma na kibinafsi."  Ilisoma taarifa katika barua ya wizara ya afya kwa kamati ya afya ya bunge.

Vile vile taifa la Kenya lina wataalamu 5 pekee wa upasuaji wa maradhi ya Endometriosis.

Majibu ya wizara ya afya yaliendelea kusema kuwa serikali imewekeza katika mashine maalum ya kuchunguza viungo  vitakavyotumika na wataalamu wa afya ya wanawake.

Hata hivyo wabunge walionyesha kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na wizara ya afya.

Dkt. Pukose  alisema wizara ya afya ina mipango ya kuanzisha vituo maalum vya Endometriosis kutoa matibabu, kutoa mafunzo kwa wataalamu zaidi na kuhakikisha dawa za kupambana na Endometriosis zinapatikana chini ya mamlaka ya afya kwa umma (SHA).

Aidha wabunge wa kike walighadhabishwa na taarifa kuwa ni hospitali mbili pekee nchini zina mashine maalum ya kuchunguza Endometriosis.

Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Mombasa Zamzam Mohamed aliitaka wizara ya afya kuwajibika ili kuwasadia wanawake wachanga  wanaougua Endometriosis kuwacha kutumia dawa za kienyeji.

Dkt. Pukose alipendekezea bunge kuhakikisha kwamba kila kaunti ina vifaa vinavyohitajika na kutoa mafunzo kwa madaktari wa magonjwa ya wanawake.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa ni hospitali ya rufaa na mafunzo ya Moi jijini Eldoret na hospitali kuu ya Kenyatta  zilizo na vifaa vya kuchunguza na kutibu maradhii ya Endometriosis nchini Kenya.