Fahamu kwa nini KQ imewaagiza wanaosafiri Jumanne kufika JKIA saa 4 mapema

KQ pia iliwatahadharisha wateja wake kutarajia kucheleweshwa kwa kuondoka na kuwasili kwa ndege zao.

Muhtasari

•Shirika hilo liliwataka wateja wake kupanga safari yao mapema na kufika katika uwanja wa ndege angalau saa nne mapema.

•Shirika hilo limewahakikishia wateja na wafanyakazi wake usalama wao na kuomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

Ndege ya Kenya Airways
Image: MAKTABA

Shirika kuu la usafiri wa anga nchini Kenya, Kenya Airways almaarufu KQ,  limetoa notisi kwa wateja wake wanaopanga kusafiri kupitia uwanja wa ndege wa JKIA mnamo Jumanne, Julai 23.

Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni, shirika hilo la usafiri liliwataka wateja wake kupanga safari yao mapema na kufika katika uwanja wa ndege angalau saa nne mapema.

Walidokeza kuhusu uwezekano wa kutatizwa kwa trafiki katika barabara kuu zinazoelekea JKIA, suala ambalo linaweza kuathiri harakati ndani na nje ya uwanja wa ndege.

"Kwa sababu ya matatizo ya trafiki yanayotarajiwa katika barabara kuu zinazoelekea JKIA mnamo Jumanne tarehe 23 Julai 2024, wateja wanashauriwa kufika katika uwanja wa ndege angalau saa nne (4) kabla ya muda wa kuondoka kwa ndege yao. Wateja pia wanahimizwa kupanga muda wa ziada ili kuepuka ucheleweshaji unaoweza kutokea wakiwa njiani kuelekea uwanja wa ndege," KQ ilisema katika taarifa.

Shirika hilo hata hivyo limewahakikishia wateja na wafanyakazi wake usalama wao na kuomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

"Wateja wanaosafiri wanaweza kuingia katika uwanja wa ndege mapema kama saa 4 kabla ya ndege kuondoka; mtandaoni kupitia www.kenya-airways.com au kwenye vifaa vyao vya rununu kupitia programu ya KQ Mobile kutoka saa 30 hadi dakika 90 kabla ya kuondoka kwa ndege," taarifa hiyo. soma zaidi.

KQ pia iliwatahadharisha wateja wake kutarajia kucheleweshwa kwa kuondoka na kuwasili kwa safari zao za ndege.

"Wakati tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha safari zetu za ndege zinaondoka na kufika kwa wakati uliopangwa, wateja wanashauriwa kutarajia kucheleweshwa kwa muda wao wa kuondoka na kuwasili ambao unaweza kuathiriwa na usumbufu huu wa trafiki," walisema.

Usumbufu wa trafiki unaotarajiwa ulitangazwa kwa Jumanne pekee.