"Ilikuwa kazi ngumu!" Chebukati atoa kauli ya mwisho huku akiaga afisi ya IEBC

"Ninaiacha IEBC ikiwa na miundo thabiti ya utawala na sekretarieti thabiti ya kudumu," alisema.

Muhtasari

•Muhula wa Chebukati katika tume ya uchaguzi nchini Kenya ulikamilika jana, Januari 17 baada ya kuwa mwenyekiti kwa miaka 6.

•Pia aliwashukuru wafanyikazi wa IEBC kwa kazi yao na  kujitolea kwao licha ya mazingira magumu yaliyowazunguka.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati
Image: MAKTABA

Aliyekuwa mwenyekiti wa tume ya IEBC Wafula Chebukati amewaaga Wakenya kwaheri huku akielekea nyumbani baada ya kustaafu.

Muhula wa Chebukati katika tume ya uchaguzi nchini Kenya ulikamilika jana, Januari 17 baada ya kuwa mwenyekiti kwa miaka 6.

Chebukati sasa amejivunia kazi yake katika tume hiyo na kuwashukuru Wakenya kwa kumpa fursa ya kuwatumikia.

"Bila shaka ilikuwa kazi ngumu, lakini nilitumikia nchi yangu kwa uwezo wangu wote na kwa mujibu wa kiapo nilichokula," Chebukati alisema katika taarifa yake ambayo alitoa  siku ya Jumatano asubuhi.

Aliongeza, "Ninaiacha IEBC ikiwa na miundo thabiti ya utawala na sekretarieti thabiti ya kudumu."

Pia aliwashukuru wafanyikazi wa IEBC kwa kazi yao na  kujitolea kwao licha ya mazingira magumu yaliyowazunguka.

"Ninyi ndio mashujaa wa kweli," aliwaambia.

Pia alishauri tume inayokuja kuwa uaminifu kwa sheria ndio ufunguo wa mafanikio kwa chombo hicho cha uchaguzi.