Mwanadada asimulia alivyoambukizwa Ukimwi katika mashindano ya Safari Rally

Grace alisema alimsihi mwanamume huyo kutumia kinga ila hakumsikia.

Muhtasari

•Mwanamke huyo aliyejitambuisha kama Grace alisema kwamba aliambukizwa VVU na mwanamume ambaye alimkabidhi shilingi 10,000 baada ya kushiriki naye tendo la ndoa.

• Tangu wakati huo maisha yake yalibadilika kabisa na kwa sasa anapitia mengi.

Mwanamke mwenye huzuni
Mwanamke mwenye huzuni
Image: HISANI

Mwanamke mmoja amejitokeza waziwazi na kusimulia yaliyompata baada ya kuambukizwa virusi vya ukimwi na mwanamume ambaye walipatana naye kwenye mashindano ya Safari Rally yaliyofanyika mapema mwaka mjini Naivasha.

Katika mahojiano na Wanjiku Tales, mwanamke huyo aliyejitambuisha kama Grace alisema kwamba aliambukizwa VVU na mwanamume ambaye alimkabidhi shilingi 10,000 baada ya kushiriki naye tendo la ndoa.

Alisema wakati ambapo madereva wa Safari Rally walikuwa wakionyesha weledi na ushupavu wao wa ranga ranga, alijifikisha katika eneo hilo na kuwatafuta wateja huku akiandamana na rafiki yake.

Alifanikiwa kupata mteja ambaye alimwahidi malipo ya shilingi 5,000 kwa usiku mmoja. Asubuhi iliyofuata, jamaa huyo alimlipa na kumlazimisha kumeza dawa za kuzuia ujauzito.

Alimsihi mwanamume huyo kutumia kinga ila hakusikiliza wala kuzingatia matatizo ambayo huenda yangewapata.

Baada ya miezi kadhaa alianza kujihisi ukosefu wa nguvu mwilini na kuamua kwenda kumwona daktari kujua hali yake ya afya. Daktari walimpa dawa alizozimeza kwa siku 7 na kujihisi afadhali.

Lakini baadaye alianza kuhisi maumivu yamezidi ikambidi amwone daktari kwa mara ya pili jambo lililomfanya daktari kumshauri afanyiwe vipimo vya ukimwi. Grace alipatwa na huzuni na wasiwasi mwingi wakati daktari alimpa habari hizo. 

Tangu wakati huo maisha yake yalibadilika kabisa na kwa sasa anapitia mengi.

Grace ambaye alijawa na majuto alisema, alizaliwa na kulelewa eneo la Nyahururu, na maisha yake yalianza kwenda kombo baada ya kifo cha mamake ambaye aliwaaga akiwa na umri wa miaka 5.

Alisema alijitosa kwenye uchuuzi wa ngono kufuatia hali mbaya ya maisha na ukosefu wa kazi ya kumletea kipato cha kuwalisha watoto wake wawili.