•Dkt Atellah alifananisha sheria hiyo mpya na wizi wa mchana na kusema kwamba itadhalilisha mfumo wa afya ya umma nchini Kenya.
•KMPDU imesema sheria hiyo ilipitishwa kwa haraka bila hata kushughulikia masuala yoyote ya NHIF ambayo yalikuwa yameibuliwa hapo awali.
Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) umekashifu Sheria mpya ya Bima ya Afya ya Jamii ya 2023.
Wakati akizungumza na wanahabari kwa niaba ya muungano huo siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu Dkt. Davji Atellah alifananisha sheria hiyo mpya na wizi wa mchana na kusema kwamba itadhalilisha mfumo wa afya ya umma nchini Kenya.
Atellah alibainisha kulikuwa na ukosefu wa kuzingatiwa kwa memo zilizowasilishwa na muungano na kupuuzwa kwa mapendekezo yao katika sheria mpya.
Muungano huo ulibainisha kuwa Sheria hiyo ilipitishwa kwa haraka bila hata kushughulikia masuala yoyote ya NHIF ambayo yalikuwa yameibuliwa hapo awali. Walitaja hili kama mgao usio sahihi wa makusudi wa rasilimali na serikali, na kuongeza kuwa ni njama ya kuwanyonya raia wa Kenya.
“Nchini Kenya, asilimia 80 ya watu wetu wanafanya kazi katika sekta isiyo rasmi na sheria hii itawabagua kwa kuwafanya wachangie mapema mchango wote wa mwaka tofauti na wenzao walioajiriwa rasmi ambao watachangia kila mwezi. Sheria hiyo alafu inadai kuponya dhuluma hii kwa serikali kuahidi kuwapa ‘bidhaa za fedha za hali ya juu’ (tafsiri kama mikopo) ili kuwasaidia kulipa, kwa manufaa ya nani?” Dkt Atellah alisema.
Aliongeza, "Tunawaomba Wakenya wote waseme Hapana na wajiunge nasi katika kupitisha ujumbe wazi kwamba hatufurahishwi na maendeleo haya yaliyojificha katika lugha ya maua ya utoaji wa huduma za afya kwa wote."
Katibu Mkuu huyo pia alibainisha kuwa licha ya Sheria hiyo kubainisha wazi kuwa kanuni zake zitatengenezwa na Bodi ya Mamlaka ya Afya ya Jamii, kanuni hizo tayari zinatengenezwa bila bodi hiyo kuwepo na bila michango ya pande zote ikiwemo Baraza la Magavana ambao ni wadau muhimu kwani afya ni kazi iliyogatuliwa.
“Tunataka hazina hiyo itolewe kwa kaunti na Tume ya Ugavi wa Mapato na isisimamiwe na Mamlaka ya Afya ya Jamii kwani hii itadhoofisha ugatuzi na kuathiri utoaji wa huduma kwa ucheleweshaji wa kudumu kama tulivyoona na pesa zinazokusudiwa kwa sekta ya elimu. Tunatoa wito kwa Magavana kuungana nasi katika harakati hizi za kutafuta fedha kufuata kazi,” alisema.
Dkt Attelah hakumaliza hotuba yake kwa vyombo vya habari bila kutoa tishio, akionya kwamba muungano huo hautakubali sheria hiyo.
"Tunataka kuwaahidi wachoraji wa wizi huu wa mchana kwamba hatutakubali majaribio yoyote ya kurudisha mafanikio ambayo tumepata kama nchi kuhusu ufadhili wa afya," alisema.
Sheria hiyo mpya, pamoja na mambo mengine, ilianzisha Mamlaka ya Bima ya Hifadhi ya Jamii kuchukua nafasi ya Mfuko wa Taifa wa Bima (NHIF). Pia ilianzisha makato ya ushuru ya lazima ya 2.75%, kwa Wakenya wanaolipwa, kusaidia kufadhili shirika hilo jipya.